Hamia kwenye habari

DESEMBA 23, 2020
URUSI

Mahakama ya Urusi Yakataa Rufaa ya Ndugu Khasan Kogut

Mahakama ya Urusi Yakataa Rufaa ya Ndugu Khasan Kogut

Desemba 23, 2020, Mahakama ya Eneo la Kemerovo ilikataa ombi la rufaa la Ndugu Khasan Kogut. Hukumu yake ya awali ya kifungo cha nje cha miaka miwili na nusu itaanza kutumika sasa. Hatahitaji kwenda gerezani wakati huu.

Ingawa Ndugu Khasan amehuzunika kwamba hukumu hiyo ya kesi ya uhalifu imemharibia rekodi yake akiwa raia, anafarijika kujua kwamba amedumisha utimilifu wake na kwamba ana kibali cha Yehova. Yekaterina, mke wa Khasan, pamoja na Timofey, mwana wao mwenye umri wa miaka minane, wameazimia kuendelea kumtumikia Yehova wakiwa familia.

Katika maneno yake ya mwisho akiwa mahakamani Septemba 10, 2020, Khasan alisema hivi kwa ujasiri: “Sitaikana imani yangu katika Yehova Mungu, na ninaona jitihada za kunilazimisha kufanya hivyo kuwa uhalifu! Hayo ni mambo ninayoamini kwa uthabiti. Hali yoyote nitakayokabili iwe ni ‘kifo wala uzima wala malaika wala serikali wala mambo yaliyopo sasa wala mambo yatakayokuja wala nguvu wala kimo wala kina wala uumbaji mwingine wowote havitaweza kututenga na upendo wa Mungu ulio katika Kristo Yesu Bwana wetu.’”—Waroma 8:38, 39.