APRILI 6, 2021
URUSI
Mahakama ya Urusi Yamhukumu Ndugu Aleksandr Shcherbina Miaka Mitatu Gerezani
HABARI ZA KARIBUNI | Mahakama ya Rufaa ya Urusi Yapunguza Kifungo cha Gereza cha Ndugu Aleksandr Shcherbina
Juni 24, 2021, Mahakama ya Eneo la Krasnodar iliunga mkono uamuzi wa kumfunga gerezani Ndugu Aleksandr Shcherbina lakini ikapunguza kifungo chake cha awali cha miaka mitatu gerezani kuwa cha miaka miwili.
Hukumu
Aprili 6, 2021, Mahakama ya Wilaya ya Abinskiy katika Eneo la Krasnodar ilimhukumu Ndugu Aleksandr Shcherbina miaka mitatu gerezani. Alipelekwa gerezani moja kwa moja kutoka mahakamani. Aleksandr atakata rufaa uamuzi huo.
Maelezo Mafupi Kumhusu
Aleksandr Shcherbina
Alizaliwa: 1976 (Kholmskaya, Eneo la Krasnodar)
Maisha Yake: Alifiwa na wazazi wote wawili. Alifanya kazi akiwa dereva wa lori, mekanika, na seremala
Alipokuwa kijana alifurahia kucheza mpira wa vikapu na wa miguu. Alipokuwa na umri wa miaka 20 hivi alijifunza Biblia na Mashahidi wa Yehova. Baada ya kujifunza kuhusu utimizo wa unabii, alisadikishwa kwamba Biblia ni Neno la Mungu. Alibatizwa mnamo 1999
Historia ya Kesi
Wenye mamlaka katika Eneo la Krasnodar walifanya msako mara mbili katika nyumba ya Ndugu Aleksandr Shcherbina, Aprili na Desemba 2020. Pindi zote mbili, Aleksandr alihojiwa na pia Biblia yake pamoja na vifaa vyake vya kielektroni vilichukuliwa.
Kesi ya uhalifu dhidi ya Aleksandr ilianza kusikilizwa Machi 17, 2021, katika Mahakama ya Wilaya ya Abinskiy. Kesi ya Aleksandr ilimalizwa upesi, kama kesi nyingine za ndugu zetu zilizofanywa katika mahakama hiyo.
Aleksandr alisema hivi kwa ujasiri alipokuwa mahakamani: “Ukweli ni kwamba nimeshtakiwa kwa kumwamini Mungu na kuendelea kuwa Shahidi wa Yehova, yaani, kwa sababu ya kutumia haki yangu inayolindwa na Kifungu cha 28 cha Katiba ya Shirikisho la Urusi. Imani yangu ya kidini inategemea Biblia, na kwa msingi huo, ni tofauti kabisa na ufafanuzi wa mtu aliye na msimamo mkali.”
Tunamshukuru Yehova kwamba ndugu na dada zetu nchini Urusi wanaendelea kuwa mifano mizuri ya ujasiri na imani. Tunajua kwamba uvumilivu wao katika kufanya “mapenzi ya Mungu” kutawaletea baraka nyingi za Yehova.—Waebrania 10:36.