Hamia kwenye habari

Aleksandr na Anna Solovyev

JULAI 5, 2019
URUSI

Mahakama ya Urusi Yamhukumu Ndugu Aleksandr Solovyev

Mahakama ya Urusi Yamhukumu Ndugu Aleksandr Solovyev

Alhamisi, Julai 4, 2019, Mahakama ya Wilaya ya Ordzhonikidzevskiy katika jiji la Perm’ nchini Urusi ilitangaza hukumu dhidi ya Ndugu Aleksandr Solovyev na kumtoza faini ya rubo 300,000 (Dola 4,731 za Marekani).

Ndugu Solovyev alikamatwa Mei 22, 2018 muda wa jioni kwenye kituo cha garimoshi, baada ya kuwasili kutoka nje ya nchi akiwa na mke wake, Anna. Polisi walimfunga pingu Ndugu Solovyev na kumweka mahabusu kwa muda. Dada Solovyev pia alikamatwa na polisi lakini wakaondoka naye kwenye gari tofauti na lililombeba mume wake. Maofisa walifanya msako katika nyumba yao usiku kucha—wakachukua picha, vifaa vya kielektroni, na Biblia kadhaa.

Baada ya kuhojiwa, Dada Solovyev aliachiliwa huru bila kushtakiwa. Hata hivyo, kesi ya uhalifu ilifunguliwa dhidi ya Ndugu Solovyev, na Mei 24, akawekwa kwenye kifungo cha nyumbani hadi Novemba 19, 2018. Huku akisubiri kesi, aliagizwa azingatie vizuzi alivyowekewa.

Mawakili wa Ndugu Solovyev watakata rufaa ya hukumu hiyo. Vilevile wamefungua mashtaka kwenye Kitengo cha Umoja wa Mataifa Kinachoshughulikia Wafungwa Wanaohukumiwa Isivyo Haki.

Mateso yanapozidi kuongezeka katika maeneo kama vile Urusi, ‘hatuogopeshwi kamwe’ na wapinzani wetu. Tunaamini kwamba Yehova ataendelea kutupa sisi sote kile tunachohitaji ili tuvumilie hadi siku yake kuu ya wokovu itakapofika.—Wafilipi 1:28