MACHI 20, 2019
URUSI
Mahakama ya Urusi Yamwachilia Shahidi Mmoja wa Yehova Kati ya Watatu Waliokuwa Kizuizini Huko Surgut, Urusi
Machi 7, 2019, Mahakama ya Rufaa ya Khanty-Mansiysk, Urusi, ilifuta uamuzi wa Mahakama ya Mwanzo ya Jiji la Surgut wa kumweka Ndugu Artur Severinchik kizuizini. Hivyo alitolewa kizuizini tarehe 15 Machi.
Ndugu Severinchik ni mmoja kati ya ndugu watatu waliokuwa kizuizini tangu Februari 17, baada ya uvamizi uliofanyika katika majiji ya Surgut and Lyantor. Mahakama imekataa kuwaachilia huru ndugu wale wengine wawili, Yevgeniy Fedin na Sergey Loginov.
Serikali mbalimbali na vituo vya habari vimeelekeza fikira zao kwenye tukio hili. Mahakama ya Ulaya ya Haki za Kibinadamu (ECHR) imeagiza Ndugu Loginov achunguzwe na daktari ambaye si wa serikali kwa kuwa alitendewa vibaya kimwili alipokuwa kizuizini.
Tunafurahi kwamba Ndugu Severinchik aliachiliwa huru. Tunaendelea kusali kwamba ndugu zetu waliofungwa nchini Urusi wamtumaini Yehova, na wakumbuke kwamba kwa msaada wake, ‘hawatatikiswa.’—Zaburi 16:8.