Hamia kwenye habari

Ndugu Nikolay Kuzichkin (kushoto) na Vyacheslav Popov (kulia)

DESEMBA 18, 2020
URUSI

Mahakama ya Urusi Yawahukumu Ndugu Nikolay Kuzichkin na Ndugu Vyacheslav Popov

Mahakama ya Urusi Yawahukumu Ndugu Nikolay Kuzichkin na Ndugu Vyacheslav Popov

Hukumu

Desemba 18, 2020, Mahakama ya Wilaya ya Khostinskiy ya Jiji la Sochi iliwahukumu Ndugu Nikolay Kuzichkin na Ndugu Vyacheslav Popov. Mahakama imemhukumu Nikolay kifungo cha mwaka mmoja na mwezi mmoja gerezani na Vyacheslav mwaka mmoja na miezi kumi. Hata hivyo, kwa kuwa walifungwa mahabusu, hukumu zao zinaonwa kuwa zimekamilishwa. Vyacheslav, ambaye bado yuko mahabusu, anatarajiwa kuachiliwa huru mara tu hukumu itakapotekelezwa. Nikolay ameachiliwa huru kutoka katika kifungo cha nyumbani.

Maelezo Mafupi Kuwahusu

Nikolay Kuzichkin

  • Alizaliwa: 1951 (Eneo la Kostroma)

  • Maisha Yake: Baada ya kumaliza masomo katika shule ya muziki, alianza kazi yake akiwa mtengenezaji piano. Yeye na mke wake, Olga, wana watoto watatu wa kiume. Pia, ni mtaalamu wa kufuga nyuki

    Alianza kujifunza Biblia na Mashahidi wa Yehova mapema katika miaka ya 1990. Kuona unabii wa Biblia ukitimizwa kulimchochea kujiweka wakfu na kubatizwa mnamo 1993

Vyacheslav Popov

  • Alizaliwa: 1974 (Tomsk)

  • Maisha Yake: Amekuwa msanii tangu utotoni, akawa mtaalamu wa mapambo ya ndani ya nyumba. Alikutana na mke wake, Yuliya, walipokuwa chuo. Walifunga ndoa mnamo 1998 na wana binti mmoja na wana wawili. Alihamia Sochi mnamo 2010. Familia yao hufurahia kuteleza kwenye barafu na kwenda matembezi baharini

    Yuliya ndiye aliyeanza kujifunza Biblia na Mashahidi wa Yehova. Baba ya Vyacheslav alipokufa, Vyacheslav alifarijiwa na kweli zilizo katika Biblia. alibatizwa mnamo 2004

Historia ya Kesi

Jioni ya Oktoba 10, 2019, vikosi vya maofisa wa kitengo cha upelelezi, waliokuwa na mbwa, walivamia nyumba 36 za Mashahidi wa Yehova katika eneo la Sochi, Urusi.

Vijana kwa wazee walilazimishwa kulala chini nyumba zao zilipokuwa zikifanyiwa msako. Simu za mkononi, tablet, kompyuta, machapisho, vitabu vya kuandikia, na hata postikadi zilichukuliwa. Hata maofisa hao walipandikiza machapisho yaliyopigwa marufuku katika nyumba fulani. Kwa sababu hiyo, maofisa hao waliwakamata Ndugu Nikolay Kuzichkin na Vyacheslav Popov. Siku iliyofuata, ndugu hao wawili walipelekwa mahabusu.

Ndugu Kuzichkin ana matatizo kadhaa makubwa ya afya. Mahakama ilikataa tena na tena maombi yake ya kupata msaada wa kitiba, ikisema kwamba hali yake haikupatana na “orodha ya magonjwa yanayomzuia mtu kuzuiliwa.” Afya ya Nikolay ilizidi kuzorota kwa sababu aliwekwa katika jela iliyokuwa na wafungwa wengi sana waliokuwa wakivuta sigara.

Licha ya hali zilizohatarisha uhai wake alipokuwa akizuiliwa, Nikolay anasema hivi: “Kufungwa ni kama eksirei. Kunasaidia kufunua sifa za ndani za Mkristo, au hata kuonyesha ikiwa ana sifa hizo au la.” Badala ya kujikazia fikiria, Nikolay alijulikana kuwa mwanamume mwenye amani na fadhili anayejitahidi kuwasaidia wafungwa wenzake waliokata tamaa na walio na mawazo ya kujiua.

Aprili 22, 2020, baada ya muda wake wa kukaa mahabusu kuongezwa mara sita, Nikolay alihamishwa kutoka mahabusu na kupewa kifungo cha nyumbani. Alikuwa dhaifu sana hivi kwamba hangeweza kusimama. Hapo tu ndipo hatimaye Nikolay aliruhusiwa kupata matibabu.

Muda wa Vyacheslav kukaa mahabusu uliongezwa mara 14, na hivyo alitenganishwa na familia yake kwa zaidi ya mwaka mzima.

Tunawashukuru Nikolay na Vyacheslav kwa mifano yao ya imani na azimio la kutegemeza enzi kuu ya Yehova. Wamekuwa wakiishi kupatana na maneno ya Zaburi 16:8: “Ninamweka Yehova mbele yangu daima. Kwa sababu yuko mkono wangu wa kulia, sitatikiswa kamwe.”