AGOSTI 11, 2020
URUSI
Maofisa wa Marekani na Ulaya Washutumu Vikali Mateso Dhidi ya Mashahidi wa Yehova Nchini Urusi
Marekani na nchi 30 katika bara la Ulaya zimeshutumu vikali minyanyaso na mateso dhidi ya ndugu zetu nchini Urusi. Shutuma hizo za kimataifa dhidi ya Urusi zilitolewa wakati wa mkutano ulioandaliwa na Shirika la Usalama na Ushirikiano wa Ulaya a (OSCE) uliofanyika Julai 23, 2020.
Akizungumza mbele ya maofisa katika mkutano huo, mshauri wa Tume ya Marekani ya Shirika la Usalama na Ushirikiano wa Ulaya, Bi. Lane Darnell Bahl, alisema hivi: “Marekani pamoja na wawakilishi wa nchi mbalimbali leo hii tumezungumza na tutaendelea kuzungumza kuhusu taarifa zenye kusikitisha za hali ya Mashahidi wa Yehova nchini Urusi wanaoteswa kimakusudi, kwa kuvamiwa nyumba zao, kuwekwa mahabusu bila sababu, kufanyiwa uchunguzi wa kihalifu, na hata kufungwa kwa miaka sita.”
Maofisa hao walisikitishwa sana pia na taarifa za hivi karibuni za kwamba wenye mamlaka nchini Urusi katika Eneo la Voronezh, walivamia nyumba zaidi ya 100 za Mashahidi wa Yehova. “Ukubwa wa kampeni za kuwanyanyasa washiriki wa kikundi hiki kidogo cha dini chenye amani unashtua sana,” akasema Bi. Bahl.
Katibu mkuu msaidizi wa Wajumbe wa Uingereza, Bi. Nicola Murray, alizungumzia pia masikitiko yake kwa kusema: “Ongezeko la upekuzi na uvamizi mkubwa wa nyumba, unatokeza wazo la kwamba kuna kampeni iliyopangwa ili tu kuwanyanyasa Mashahidi wa Yehova.” Bi. Murray aliendelea kusema: “Huo unaoitwa eti ‘ushahidi’ unaotumiwa dhidi ya wanaofanyiwa upelelezi, unatia ndani kushiriki kwa ukawaida katika shughuli za kidini.”
Kwa kuongezea, Bi. Bahl alifichua madai ya uwongo ya wenye mamlaka wa Voronezh kwamba Mashahidi waliofungwa walikuwa na kosa linalohusiana na “kupanga njama.” Njama hizo zilihusisha kutunza ripoti na nyaraka zingine katika mfumo wa kielektroni, kupanga vikundi, na kutumia video mtandaoni ili kufanya mikutano. Bi. Bahl alisema mashtaka hayo yanayotolewa na mamlaka za Urusi ni ya “kipuuzi na ya aibu.” Alisema hivi: “Ikiwa hizo ni njama basi mimi ninazitumia kila siku.” Alisema pia kwamba Wajumbe wa Urusi wanaoshiriki katika mkutano huo wa OSCE kwa kutumia video mtandaoni, walikuwa pia na “makosa kwa kufanya hivyo.”
Katika maelezo ya pamoja, washiriki kutoka nchi 27 za Umoja wa Ulaya (EU), pamoja na washiriki wengine nane kutoka nchi ambazo si wanachama, walisema hivi: “Tumewasikia Wajumbe wa Urusi wakidai zaidi ya mara moja mbele ya Baraza la Kudumu kwamba Mashahidi wa Yehova wanaweza, na wataendelea kuwa na uwezo wa kuabudu kwa uhuru, na kwamba kuna uhuru wa dini au imani katika Shirikisho la Urusi. Hata hivyo, tunaendelea kusikia taarifa nyingi kuhusu nyumba kuvamiwa, vifungo, na uchunguzi wa kihalifu dhidi ya Mashahidi wa Yehova. Madai hayo yanatofautiana sana na yale yaliyosemwa na Wajumbe wa Urusi.”
Wajumbe wa Ulaya walisema hivi pia: “Watu wote, kutia ndani Mashahidi wa Yehova, wanapaswa kuwa na uwezo wa kufurahia kwa amani haki zao za binadamu, kutia ndani haki ya kuabudu kwa uhuru, kukusanyika na kushirikiana kwa uhuru, na uhuru wa usemi, bila kubaguliwa, kama vile Katiba ya Shirikisho la Urusi inavyosema [na] kupatana na madhumuni na malengo ya Shirika la Usalama na Ushirikiano wa Ulaya chini ya sheria ya kimataifa.”
Bi. Murray alimalizia maelezo yake kwa niaba ya Uingereza kwa kuisihi Urusi iache kuwanyanyasa Mashahidi wa Yehova.
Bi. Bahl ameisihi Urusi: (1) iache kufanya uchunguzi wa kihalifu dhidi ya Mashahidi wa Yehova, (2) irudishe jengo la makao makuu ya Mashahidi wa Yehova nchini Urusi, na (3) iwaachilie mara moja Mashahidi wote waliofungwa gerezani.
Hii si mara ya kwanza kwa mashirika ya kimataifa kushutumu vikali Urusi kwa kuwanyanyasa ndugu zetu. Urusi imewahi kuonywa. Jumuiya ya kimataifa inajua kwamba nchi hiyo inawatesa vibaya sana ndugu na dada zetu. Jambo la muhimu zaidi, tuna uhakika kwamba Yehova anajua mambo ambayo ndugu na dada zetu nchini Urusi wanakabili. (Zaburi 37:18) Bila shaka, Baba yetu wa mbinguni mwenye upendo ataendelea kuwabariki kwa sababu ya uaminifu, ujasiri, na uvumilivu wao.—Zaburi 37:5, 28, 34.
a OSCE ina wajibu wa kuhakikisha kwamba haki za binadamu zinalindwa. Baraza la Kudumu la OSCE ndilo hufanya maamuzi yote muhimu.