Hamia kwenye habari

Kushoto hadi kulia: Anatoly Razdobarov akiwa na mke wake Greta, na Nikolay Merinov na mke wake, Liliya, kabla ya kushambuliwa na maofisa wa usalama wa Urusi

OKTOBA 10, 2021
URUSI

Maofisa wa Urusi Wawashambulia Wenzi wa Ndoa

Maofisa wa Urusi Wawashambulia Wenzi wa Ndoa

Jumatatu, Oktoba 4, 2021, maofisa wenye silaha wa kitengo cha pekee nchini Urusi kinachoitwa OMON a walimshambulia Ndugu Anatoly Razdobarov na mke wake Greta na pia wakamshambulia Ndugu Nikolay Merinov na mke wake Liliya. Mashambulizi hayo ya kikatili yalitokea wakati maofisa hao wa usalama walipovamia nyumba 12 za Mashahidi wa Yehova katika jiji la Irkutsk. Maofisa hao waliwaweka kizuizini ndugu wengine kadhaa wakati wa mashambulizi hayo.

Saa 12:00 alfajiri, maofisa hao waliingia kwa nguvu ndani ya nyumba ya Anatoly na Greta. Walimburuta Greta kwa nywele zake na kumpeleka katika chumba kingine, wakamfunga mikono yake nyuma ya mgongo, na kumpiga tena na tena.

Wakati huo, Anatoly aliangushwa chini, akafungwa pingu mgongoni, na kupigwa teke kichwani na tumboni. Maofisa walishika mikono yake iliyofungwa mgongoni na kumnyanyua kwa nguvu. Hilo lilimfanya Anatoly apate uchungu mwingi kwa sababu uzito wote wa mwili wake ulitegemezwa kwenye mabega yake. Maofisa walimpiga kwenye mikono yake wakimlazimisha akubali kwamba alikuwa ametenda uhalifu na pia awape habari kuwahusu ndugu wengine. Mbali na hilo, maofisa walimtesa zaidi kwa kujaribu kulazimisha chupa iingie kwenye matako yake. Uvamizi huo nyumbani kwa akina Razdobarov uliendelea kwa zaidi ya saa nane.

Maofisa walipovamia nyumba ya Nikolay na Liliya Merinov, walianza kwa kumpiga Nikolay usoni kwa kitu kizito ambacho ni butu. Alianguka chini na kupoteza fahamu. Aliporudiwa na fahamu, alitambua kwamba kulikuwa na ofisa aliyeketi juu yake akimpiga. Ofisa huyo alivunja meno ya mbele ya Nikolay. Mke wake Liliya aliburutwa kwa nywele zake kutoka kitandani na kufungwa pingu. Kisha maofisa wakamshambulia vibaya tena na tena kabla ya kumruhusu avae nguo vizuri.

Kulingana na Sheria ya Urusi, matumizi hayo mabaya ya mamlaka ni uhalifu. Mbali na hilo, Shirikisho la Urusi linapaswa kutii sheria za kuwalinda watu wasiteswe zilizowekwa na mashirika kadhaa ya kimataifa. Kwa sababu hiyo, wenzi hao wa ndoa watatumia njia zote za kisheria katika mahakama nchini Urusi na katika mahakama za kimataifa, ili kupambana na ukatili huo waliotendewa.

Siku moja baada ya maofisa kuvamia nyumba 12 huko Irkutsk na kushambulia familia mbili, ndugu na dada 300 hivi walifika kwenye Mahakama ya Wilaya ya Oktyabrskiy iliyoko Irkutsk ili kuwaunga mkono ndugu wengine sita walipelekwa mahabusu

Siku mbili baada ya uvamizi huo, mahakama iliagiza ndugu sita wawekwe mahabusu: Yaroslav Kalin, Sergey Kosteev, Nikolay Martynov, Mikhail Moish, Aleksey Solnechny, na Andrey Tolmachev. Ndugu na dada 300 walisafiri kwenda mahakamani ili kuwaunga mkono kwa amani waabudu wenzao waliotendewa ukosefu wa haki.

Tungependa kuwaambia ndugu na dada zetu wote nchini Urusi maneno haya yaliyoongozwa na roho ambayo Paulo aliwaandikia Wathesalonike: “Tunajivunia ninyi kati ya makutaniko ya Mungu kwa sababu ya uvumilivu na imani yenu katika mateso yenu yote na taabu mnayopata.”​—2 Wathesalonike 1:4.

a Kitengo cha Pekee cha Ulinzi wa Taifa cha Urusi