NOVEMBA 6, 2020
URUSI
Mashirika ya Kimataifa Yapinga Hatua ya Urusi ya Kuwanyanyasa Mashahidi wa Yehova
“Ukosefu mbaya sana wa haki.”—Gayle Manchin, Mwenyekiti wa USCIRF
Maofisa kutoka Ulaya na Marekani wanaendelea kukemea vikali kitendo cha Urusi cha kuendelea kuwanyanyasa Mashahidi wa Yehova nchini humo.
Tume ya Uhuru wa Kidini wa Kimataifa ya Marekani (USCIRF)
Mwenyekiti Gayle Manchin, katika maelezo rasmi aliyotoa Oktoba 27, 2020. aliendelea kusema: “USCIRF imeshtushwa na namna serikali ya Urusi inavyomtendea Dennis Christensen. Ni wazi kwamba serikali inamchukia mwanamume huyo, ambaye kosa lake ni kufanya ibada. Badala ya kumwonyesha rehema, serikali inamtendea kama mhalifu hatari sana. Huo ni ukosefu mbaya sana wa haki.”
Mwenyekiti Manchin anamtetea Ndugu Christensen kupitia Mradi wa USCIRF unaoitwa Wafungwa wa Kidini kwa Sababu ya Dhamiri. USCIRF imekemea vikali sana mara nyingi hukumu aliyopewa Ndugu Christensen ya kufungwa gerezani kwa miaka sita.
Katika maelezo yao, USCIRF imeishutumu pia Urusi kwa kukataa kumwachilia huru mapema Ndugu Christensen. USCIRF inasema kwamba “aliruhusiwa kutoka Juni 23, [2020,] lakini uamuzi huo ulipingwa bila kukawia na mwendesha-mashtaka wa serikali. Badala ya kuachiliwa huru, Christensen alifungwa katika chumba gerezani kisichokuwa na hewa kwa madai ya kwamba alivunja sheria za gereza.”
Maelezo ya USCIRF yanamalizia kwa kurejelea Ripoti yake Mwaka wa 2020. Ripoti hiyo inashutumu serikali ya Urusi kwa “kupanga, kutekeleza na kuvunja haki ya kuabudu kwa uhuru” na inapendekeza kwamba serikali ya Marekani itoe adhabu kwa Urusi kwa kuiweka katika orodha ya “nchi inayotia wasiwasi mkubwa.”
Baraza la Haki za Kibinadamu la Umoja wa Mataifa
Katika barua ya pamoja kwa Ubalozi wa Shirikisho la Urusi katika Umoja wa Mataifa, maofisa nane wenye vyeo vya juu katika Baraza la Haki za Kibinadamu la Umoja wa Mataifa, walionyesha kushtushwa kwao kutokana na “kunyanyaswa kwa Mashahidi wa Yehova kunakoendelea katika Shirikisho la Urusi, kufungwa kwa Ofisi ya Mashahidi wa Yehova katika jiji la St. Petersburg, na kupigwa marufuku kwa vituo vyake 395 katika nchi hiyo.” Maofisa hao walikosoa kitendo cha Urusi cha kupuuza maombi kutoka mashirika ya kimataifa ya kuitaka iache kuwanyanyasa Mashahidi wa Yehova.
Maofisa wa Umoja wa Mataifa walisema kwamba sheria za msimamo mkali zisizo wazi nchini Urusi, “zimewekwa ili kuzuia shughuli yoyote ya kidini ya Mashahidi wa Yehova, kuwatia hofu, kuingilia haki yao ya kuwa na faragha kupitia uvamizi na upekuzi katika nyumba zao unaofanywa na polisi, kuwaweka kizuizini baadhi ya washiriki wake kwa lengo la kuwahoji, na katika visa fulani kuwahukumu na kuwafunga gerezani.”
Maofisa hao waliendelea kusema, “Mashahidi wa Yehova wana haki ya kuwa na uhuru wa kidini kulingana na kifungu namba 18 (1) cha ICCPR.” a Hivyo, wanalihimiza Shirikisho la Urusi “kuhakikisha kwamba Sheria ya Serikali ya Kupambana na Watu Wenye Msimamo Mkali ya mwaka wa 2002, haitumiki kuvunja haki ya kikatiba ya kila mtu ya kuwa na uhuru wa kuwa na mawazo, dhamiri, dini au imani.”
Barua hiyo pia ilifunua jinsi ndugu zetu wanavyotendewa kwa ukatili. Kwa mfano, ilitaja Mashahidi watano kutoka Saratov waliopigwa vibaya Februari 6, 2020. Barua hiyo inafafanua zaidi kwa kusema hivi: “Mashahidi wanaofungwa, mara nyingi huwekwa katika mahabusu zilizo na hali mbaya, hunyanyaswa na kutendewa kwa jeuri kwa sababu ya imani yao.”
Barua hiyo inataja kisa kingine cha mtu aliyenyanyaswa. Maofisa wa Urusi walimnyanyasa Ndugu Vadim Kutsenko Februari 10, 2020. Mamlaka za Urusi zinakataa kwamba zilimtesa Ndugu Kutsenko. Hata hivyo, maofisa wa Umoja wa Mataifa hawaamini mamlaka za Urusi, hivyo wanaendelea kuwa na “wasiwasi mkubwa na hali inayoonekana kuwa kampeni ya nchi nzima ya kuwanyanyasa Mashahidi wa Yehova kwa kudai kwamba shughuli zao zenye amani ni uhalifu.”
Halmashauri ya Mawaziri wa Baraza la Ulaya
Marufuku ya 2017 na unyanyasaji ulioanza baada ya hapo, ulikuwa chanzo cha Halmashauri ya Mawaziri wa Baraza la Ulaya b kuchunguza kwa makini ikiwa Urusi inatii maamuzi ya Mahakama ya Ulaya ya Haki za Kibinadamu katika kesi mbili dhidi ya Urusi iliyokutwa na kosa la kukiuka haki za Mashahidi wa Yehova. c Hivyo, Halmashauri ilitoa uamuzi Oktoba 1, 2020, ambapo ilitaja kuendelea kuwa na “wasiwasi mkubwa kuhusu marufuku ya jumla ya mwaka wa 2017 na ripoti zinazoshtua kutoka vyanzo mbalimbali . . . kwamba kwa sababu ya marufuku hiyo, Mashahidi wa Yehova wanaendelea kukamatwa, kufunguliwa mashtaka, na kufungwa gerezani kwa sababu tu ya kuendelea kufanya ibada yao kwa amani.”
Ili kuzuia kuvunjwa kwa haki hizo, Halmashauri inapendekeza kwamba Urusi itafute njia za kuboresha “sheria yake ya msimamo mkali wa kidini ambayo imetumika kama msingi wa kupiga marufuku na mwishowe kuwafungulia mashtaka ya uhalifu Mashahidi wa Yehova.” Kwa kuongezea, Urusi inapaswa kufikiria “kuondoa marufuku ya jumla na kusitisha kesi za uhalifu dhidi ya Mashahidi wa Yehova zilizofunguliwa kwa sababu ya kushiriki katika shughuli za kidini zenye amani.” Mwaka wa 2021, Urusi itachunguzwa tena ikiwa imetekeleza mapendekezo hayo.
Tangu mwaka wa 2017, zaidi ya ndugu na dada zetu 400 katika Urusi na Crimea, wameshtakiwa kwa uwongo kwa kosa la kuwa na msimamo mkali wa kidini. Zaidi ya Mashahidi 210 wamefungwa katika majiji 70 nchini Urusi.
“Sisi tunaliitia jina la Yehova Mungu wetu” ili aendelee kuwasaidia ndugu na dada zetu wavumilie wakiwa na subira.—Zaburi 20:2, 7.
b The Halmashauri ya Mawaziri husimamia utekelezaji wa maamuzi ya Mahakama ya Ulaya ya Haki za Kibinadamu.