Hamia kwenye habari

Mahakama ya Ulaya ya Haki za Kibinadamu (ECHR) iliyo Strasbourg, Ufaransa

JUNI 10, 2020
URUSI

Miaka Kumi Baada ya Ushindi Mkubwa wa ECHR, Urusi Bado Haitii Sheria ya Kimataifa

Miaka Kumi Baada ya Ushindi Mkubwa wa ECHR, Urusi Bado Haitii Sheria ya Kimataifa

Sasa ni miaka kumi tangu Juni 10, 2010, Mahakama ya Ulaya ya Haki za Kibinadamu (ECHR) ilipotoa uamuzi wa kwamba mamlaka za Urusi zilikiuka kwa kiasi kikubwa haki za binadamu kupitia kampeni yao ya miaka mingi ya kukandamiza ndugu zetu kwa kuwanyima haki yao ya kuabudu. Uamuzi wa ECHR ulisema Urusi ilipaswa ilipe faini kubwa na kusajili tena shirika la kidini la Mashahidi wa Yehova Local Religious Organization (LRO) la Moscow—lililofungiwa mwaka wa 2004.

Baada tu ya uamuzi huo kutangazwa, Ndugu Ivan Chaykovskiy, mwenyekiti wa Moscow Community of Jehovah’s Witnesses, alisema hivi: “Ushindi huu ni ushahidi wa kutosha unaoonyesha kwamba ubaguzi wa kidini haupatani na akili. Ni matumaini yetu kuwa kupitia uamuzi huu, wenye mamlaka wataturudishia haraka haki yetu ya kisheria na kusitisha kampeni zao za kuwatesa Mashahidi wa Yehova nchini.”

Matumaini hayo yalitoweka haraka baada ya wenye mamlaka nchini Urusi kutotii uamuzi huo wa ECHR, na kuwatesa hata zaidi ndugu zetu nchini pote. Mateso hayo yaliongezeka zaidi baada ya Mahakama Kuu ya Urusi kupiga marufuku ibada zetu tunazofanya kwa amani katika mwaka wa 2017, ukosefu huo mkubwa wa haki ulifuatiwa na ndugu wengi kukamatwa, kufunguliwa mashtaka, na kufungwa gerezani.

Ingawa miaka kumi imepita, uamuzi huo mkali wa ECHR dhidi ya Urusi bado unafaa. Mwaka 2010, ECHR ilipinga vikali mashtaka mengi ambayo mpaka leo Urusi inaendelea kutumia kushtaki waamini wenzetu wenye amani.

Kwa ufupi, ECHR ilifikia mkataa kwamba Wizara ya Sheria ya Moscow na mahakama za Moscow, hazina “msingi wa kisheria” wa kukataa kusajili tena dini ya Mashahidi wa Yehova. ECHR ilishutumu mamlaka za Moscow kwa kusema kwamba, “hawakutenda kwa nia nzuri na wamepuuza jukumu lao la kutounga mkono upande wowote na kutobagua.” Kwa kuongezea, mamlaka za Moscow zilikuwa na kosa la kuvunja mkataba wa Mahakama ya Ulaya ya Haki za Binadamu, mahakama ambayo Urusi ni mwanachama pia.

Katika mwaka huu wa 2020, bado Urusi inaendelea kunyanyasa ndugu zetu kama walivyofanya mwaka wa 2010. Rachel Denber, naibu mkurugenzi wa shirika la Human Rights Watch katika bara la Ulaya na Asia ya Kati alisema hivi Januari 9, 2020: “Utendaji wa Mashahidi wa Yehova nchini Urusi unahatarisha uhuru wao, wale wanaowatendea hivyo hawana sababu yoyote ya msingi ya kufanya hivyo.”

Kwa sababu ya ukosefu huo wa haki, tunasali tukiwa na uhakika kwamba Yehova ataendelea kuwaimarisha ndugu na dada zetu nchini Urusi ili “ [wavumilie] kikamili kwa subira na shangwe.”—Wakolosai 1:11.