OKTOBA 28, 2021
URUSI
Mwalimu Aliyestaafu Mwenye Umri wa Miaka Themanini Anakabili Mashtaka kwa Sababu ya Kuzungumzia Biblia
HABARI ZA KARIBUNI | Mahakama ya Urusi Yakataa Ombi la Rufaa la Dada Yelena Savelyeva
Februari 14, 2022, Mahakama ya Eneo la Tomsk ilikataa ombi la rufaa la Dada Yelena Savelyeva. Hatahitaji kwenda gerezani wakati huu.
Mfuatano wa Matukio
Novemba 17,2021
Mahakama ya Jiji la Severskiy ya Eneo la Tomsk ilimhukumu Dada Yelena Savelyeva kifungo cha nje cha miaka minne. Hatahitaji kwenda gerezani wakati huu. Hapo awali, mwendesha-mashtaka aliomba mahakama impige Yelena mwenye umri wa miaka 80, faini ya rubo 500,000 (dola 7,198 za Marekani)
Julai 22,2021
Mahakama ilisikiliza kesi kwa mara ya kwanza
Machi 25, 2021
Mwendesha-mashtaka nchini Urusi alimfungulia Yelena kesi ya uhalifu. Anashtakiwa kwa “kumshawishi, na kumshirikisha mtu katika utendaji wa shirika lenye msimamo mkali” chini ya Kifungu cha 282.2 cha Sheria ya Uhalifu ya Shirikisho la Urusi.
Mashtaka hayo yanategemea ushahidi wa wanawake wawili ambao Yelena alizungumza nao kuhusu Biblia: mmoja wao alikuwa ofisa wa FSB na mwingine alikuwa mfanyakazi wa Jeshi la Taifa la Urusi. Wanawake hao walijifanya kwamba wanapendezwa na ujumbe wa Biblia, ilihali walikuwa wakirekodi kwa siri mazungumzo yao pamoja na Yelena. Kisha, wakawasilisha habari kumhusu Yelena na za waamini wenzake kwa wenye mamlaka
Maelezo Mafupi Kumhusu
Tunapata ujasiri tunapoona jinsi Yelena alivyoazimia kubaki imara licha ya mateso. Tuna uhakika kwamba Yehova anawaona wale wote ‘wanaojitahidi pamoja kwa ajili ya imani ya habari njema, bila kuogopeshwa kamwe na wapinzani wao.’—Wafilipi 1:27, 28.