Hamia kwenye habari

Ndugu Aleksandr Ivshin

FEBRUARI 12, 2021
URUSI

Ndugu Aleksandr Ivshin Mwenye Umri wa Miaka Sitini na Tatu Amehukumiwa Kifungo cha Miaka Saba na Nusu Gerezani kwa Kupanga Mikutano na Kuimba Nyimbo Kupitia Mtandao

Ndugu Aleksandr Ivshin Mwenye Umri wa Miaka Sitini na Tatu Amehukumiwa Kifungo cha Miaka Saba na Nusu Gerezani kwa Kupanga Mikutano na Kuimba Nyimbo Kupitia Mtandao

Hukumu

Februari 10, 2021, Mahakama ya Wilaya ya Abinskiy katika Eneo la Krasnodar ilimhukumu Ndugu Aleksandr Ivshin. Alihukumiwa kifungo cha miaka saba na nusu gerezani. Hiyo ndiyo hukumu kali zaidi kupewa mmoja wa ndugu zetu tangu tengenezo letu lilipopigwa marufuku mwaka wa 2017.

Maelezo Mafupi Kumhusu

Aleksandr Ivshin

  • Alizaliwa: 1957 (Katav-Ivanovsk)

  • Maisha Yake: Kabla ya kustaafu alifanya kazi kwenye mashine ya vyuma, kukata miti, na akiwa injinia wa kuhakikisha usalama kiwandani. Alifunga ndoa na Galina katika mwaka wa 1974. Wana binti wawili na wajukuu wanane

    Baada ya kupatwa na ugonjwa mbaya, alianza kufikiria kuhusu kusudi la uhai. Usiku mmoja aliposoma vitabu vitatu vya Injili, akaanza kujifunza Biblia. Alibatizwa mwaka wa 1995.

Historia ya Kesi

Matatizo ya kisheria dhidi ya Mashahidi wa Yehova katika eneo la Abinsk yalianza katika mwaka wa 2015. Shirika la Kidini la Mashahidi wa Yehova lilisemwa kuwa ni “lenye msimamo mkali” na likapigwa marufuku. Aprili 23, 2020, miaka mitano baadaye, kesi ya uhalifu dhidi ya Ndugu Aleksandr Ivshin ilifunguliwa. Baadhi ya yanayodaiwa kuwa matendo ya uhalifu yaliyotajwa dhidi yake ni kupanga mikutano ya kidini na kuimba nyimbo za Ufalme kupitia video mtandaoni.

Mkazo uliotokana na upekuzi wa nyumba ya Aleksandr na Galina, ulifanya shinikizo lao la damu lipande kwa kiwango hatari sana. Miezi kadhaa baada ya upekuzi huo, gari la Aleksandr lilichukuliwa na wenye mamlaka. Licha ya hali hizo ngumu, Aleksandr ameendelea kuwa na mtazamo mzuri. Katika maelezo yake ya mwisho mbele ya mahakama, alisema hivi: “Sishangai kwamba mimi ndiye mshtakiwa katika kesi hii, kwa sababu Yesu alitabiri jambo hilo. Mathayo 10:18 inasema: ‘Nanyi mtapelekwa mbele ya magavana na wafalme kwa ajili yangu, ili kuwa ushahidi kwao na kwa mataifa.’ . . . Maneno ya Yesu hayanifanyi nishuke moyo. Badala yake yananifanya niwe na furaha kwa sababu ninaweza kuiambia mahakama hii kuhusu tumaini la wakati ujao kwa ajili ya watu wote wanaotambua uhitaji wao wa kiroho.”

Kisa cha Aleksandr na Galina kinaongezea kwenye ushahidi mkubwa ambao unatolewa nchini Urusi na katika sehemu zote za dunia. Tuna uhakika kwamba watabarikiwa sana kwa kuendelea kumtegemea Yehova.—Yeremia 17:7.