Hamia kwenye habari

Ndugu Andrzej Oniszczuk akiwa kizimbani mahakama ilipokuwa ikichunguza upya kifungo chake

AGOSTI 9, 2019
URUSI

Ndugu Andrzej Oniszczuk Anakaribia Kumaliza Mwaka Mmoja Katika Kifungo cha Upweke

Ndugu Andrzej Oniszczuk Anakaribia Kumaliza Mwaka Mmoja Katika Kifungo cha Upweke

Andrzej Oniszczuk, raia wa Poland na ambaye ni ndugu yetu mpendwa amefungwa nchini Urusi akisubiri kushtakiwa tangu maofisa wa usalama walipomkamata Oktoba 9, 2018. Hivi karibuni kifungo chake kiliongezwa kwa mara ya tano. Kifungo chake kipya kinapaswa kuisha Oktoba 2, siku chache tu kabla ya kumaliza mwaka mzima tangu alipofungwa.

Andrzej, akiwa pamoja na mke wake Anna, kabla ya kukamatwa. Mke wake hajaruhusiwa kumtembelea tangu alipokamatwa miezi kumi iliyopita

Tangu alipokamatwa, Andrzej amekuwa katika kifungo cha upweke. Haruhusiwi kulala kuanzia saa 12:00 asubuhi hadi saa 3:00 usiku. Anaruhusiwa kuoga kwa maji ya moto kwa dakika 15 mara moja tu kwa juma. Anna, mke wa Andrzej hajaruhusiwa kumtembelea kwa miezi kumi ambayo amekuwa kifungoni. Wanawasiliana tu kupitia barua. Amewasilisha mara nyingi maombi ya kumtembelea mume wake, Andrzej, lakini maombi hayo yote yalikataliwa.

Kama ilivyoripotiwa awali, Andrzej alikamatwa na polisi na maofisa waliofunika nyuso zao walipovamia nyumba yake na za wengine 18 huko Kirov. Andrzej alifunguliwa mashtaka ya kesi ya uhalifu kwa sababu ya kuimba nyimbo za Ufalme na kusoma machapisho ya kidini.

Pia, ndugu wengine wanne kutoka Kirov (Maksim Khalturin mwenye umri wa miaka 44, Vladimir Korobeynikov mwenye umri wa miaka 66, Andrey Suvorkov mwenye umri wa miaka 26, na Evgeniy Suvorkov mwenye umri wa miaka 41) walikamatwa pamoja na Andrzej mwaka uliopita na walifungwa wakisubiri kufunguliwa kwa kesi zao. Tangu wakati huo wamekuwa wakitumikia katika kifungo cha nyumbani. Kesi ya Andrzej, pamoja na ya ndugu hao wanne, inasubiri uamuzi wa Mahakama ya Ulaya ya Haki za Kibinadamu.

Mwaka huu, serikali ya Urusi imefungua kesi za mashtaka dhidi ya ndugu wengine saba kutoka Kirov—ndugu aliye na umri mkubwa zaidi ni Yevgeniy Udintsev, mwenye umri wa miaka 70. Jumla ya Mashahidi wa Yehova 12 kutoka Kirov wanakabili mashtaka ya uhalifu kwa sababu ya imani yao.

Basi, na tusisahau kamwe kikumbusho hiki kutoka katika Neno la Mungu kuwahusu Andrzej, Anna, na ndugu na dada wengine wote kutoka Urusi: “Wakumbukeni wale walio gerezani, kana kwamba mmefungwa pamoja nao, na wale wanaoteswa, kwa kuwa ninyi pia mko katika mwili.”— Waebrania 13:3.