JULAI 24, 2020
URUSI
Ndugu Dennis Christensen Arudishwa Tena Kwenye Jela ya Adhabu
Julai 15, 2020, Ndugu Dennis Christensen alirudishwa kwenye jela ya adhabu inayoitwa SHIZO kwa mara ya pili. Atabaki humo huenda hadi Julai 27. Alirudishwa siku nne tu baada ya kutolewa huko. Ikiwa atapelekwa huko kwa mara ya tatu, gereza hilo litamwona kuwa “mtu hatari anayekiuka taratibu za gereza” na kumpeleka kwenye jela ya adhabu ya pekee iliyokusudiwa hasa wahalifu sugu (EPKT) hata kwa miezi sita. Wakili wa Ndugu Christensen atakata rufaa mashtaka hayo ya hivi karibuni.
Wenye mamlaka wanamwadhibu Ndugu Christensen kwa sababu afya yake haimruhusu kufanya migawo anayopewa gerezani. Wakuu wa gereza wanasisitiza Ndugu Christensen afanye kazi katika kiwanda cha ushonaji cha gereza. Lakini afya yake imedhoofika sana tangu alipofungwa gerezani. Madaktari wa gereza wanadai kwamba ana afya kiasi cha kufanya kazi hiyo maadamu atapewa muda wa mapumziko na wa kufanya mazoezi. Hata hivyo, daktari mwingine ambaye si wa gereza hilo alimpima Ndugu Christensen mapema. Alisema kwamba afya ya Ndugu Christensen haiwezi kumruhusu kufanya kazi aliyopewa.
Katika SHIZO, wafungwa hawana ruhusa ya kununua chakula, kupiga au kupigiwa simu, kupokea wageni au mzigo wowote. Sheria inaruhusu wafungwa walio SHIZO kutembelewa na wahudumu wa kidini. Hata hivyo, Ndugu Christensen hawezi kutembelewa na wazee. Hiyo ni kwa sababu Mashahidi wa Yehova hawatambuliwi tena kuwa dini iliyoandikishwa kisheria nchini Urusi.
Kama ilivyoripotiwa Juni 23, Mahakama ya Wilaya ya Lgov ilikubali kumwachilia huru Ndugu Christensen na ikaamua kwamba muda uliobaki wa kifungo chake ufidiwe na faini. Lakini siku kadhaa baadaye, mwendesha-mashtaka alikata rufaa uamuzi huo. Inaonekana kwamba wakuu wa gereza wanashirikiana na mwendesha-mashtaka kuharibu jina zuri la Ndugu Christensen ili asiachiliwe mapema.
Ndugu Christensen pamoja na mke wake, Irina, wanajitahidi kudumisha shangwe yao. Tunatiwa moyo sana kuona jinsi Yehova anavyowasaidia watumishi wake waaminifu kuvumilia hata hali ngumu sana kuwa subira na shangwe.—Wakolosai 1:11.