MACHI 18, 2021
URUSI
Ndugu Dmitriy Maslov Anaweza Kufungwa Gerezani kwa Kuzungumzia Mambo ya Kiroho na Rafiki Zake
HABARI ZA KARIBUNI | Mahakama ya Urusi Yakataa Ombi la Rufaa
Oktoba 5, 2021, Mahakama ya Eneo la Krasnoyarsk ilikataa ombi la rufaa la Dmitriy. Faini aliyotozwa awali haijabadilishwa.
Juni 2, 2021, Mahakama ya Jiji la Minusinsk katika Eneo la Krasnoyarsk ilimhukumu Ndugu Dmitriy Maslov na kumtoza faini ya rubo 450,000 (dola 6,125 za Marekani).
Maelezo Mafupi Kumhusu
Dmitriy Maslov
Alizaliwa: 1976 (Minusinsk)
Maisha Yake: Yeye pamoja na kaka na dada yake walilelewa na mama yao. Alihitimu katika shule ya ufundi na kupata digrii ya ufugaji wa nyuki. Kwa sasa anafanya kazi akiwa fundi wa mabomba. Anapenda kuendesha baiskeli, kupiga mbizi, na kucheza ala ya muziki ya kodiani
Tangu alipokuwa na umri mdogo, alikuwa akitafuta majibu ya maswali muhimu maishani. Alipata majibu yenye kuridhisha na yaliyo wazi katika Biblia. Alibatizwa 1994. Alipoitwa akatumikie jeshini, alikataa na kuomba kufanya utumishi wa badala kwa sababu ya dhamiri yake. Alifunga ndoa na Yuliya mwaka wa 1997
Historia ya Kesi
Jioni ya Aprili 19, 2019, huko Minusinsk, wanajeshi na maofisa wa Kamati ya Uchunguzi na wa Idara ya Usalama wa Taifa (FSB), walivamia nyumba za familia tano za Mashahidi wa Yehova. Katika msako huo, ndugu mwenye umri wa miaka 76 alijeruhiwa baada ya kusukumwa na kuanguka chini. Zaidi ya ndugu na dada 30 walikamatwa ili kuhojiwa na baadaye wakaachiliwa huru. Baadaye, kesi ya uhalifu ilifunguliwa dhidi ya Dmitriy. “Kosa” lake kuu lilikuwa kupanga matembezi mlimani pamoja na rafiki zake, ambako walizungumzia mambo ya kiroho.
Dmitriy, amezuiwa kusafiri na anasubiri hukumu yake. Mama yake ambaye si Shahidi wa Yehova anaona kwamba mashtaka hayo ya uhalifu si ya haki na mwana wake hastahili kutendewa kama mhalifu. Ana uhakika kwamba mwana wake anashirikiana na dini ambayo “washiriki wake ni wenye amani.”
Dmitriy anapata faraja na ujasiri kwa kujua kwamba Yehova ‘atadhihirisha nguvu zake’ kuelekea washikamanifu wake.—2 Mambo ya Nyakati 16:9.