JANUARI 21, 2021
URUSI
Ndugu Feliks Makhammadiyev Aachiliwa Huru Kutoka Gerezani Urusi na Kuhamishiwa Uzbekistan
Desemba 31, 2020, Ndugu Feliks Makhammadiyev aliachiliwa huru kutoka gerezani nchini Urusi. Mahakama ya Wilaya ya Belyayevsky katika Eneo la Orenburg ilitoa uamuzi wa kumzuia kwa muda katika kituo cha uhamisho hadi alipopata hati zinazohitajika ili aweze kuhamishiwa katika nchi yake ya Uzbekistan. Hatua hiyo ilichukuliwa kwa sababu Urusi ilifuta uraia wake Aprili 2020. Januari 20, 2021, wenye mamlaka walihakikisha kwamba amepanda treni inayoelekea Uzbekistan. Tunafurahi kuripoti kwamba Feliks alifika salama Uzbekistan Januari 21, 2021. Mke wake, Yevgeniya, alienda Uzbekistan siku mbili kabla yake hivyo aliweza kumpokea alipofika.
Felix aliishi Urusi kwa miaka 18 hivi. Katika mwaka wa 2002, alipokuwa kijana, yeye na mama yake walihamia Saratov, Urusi wakitokea Uzbekistan. Alibatizwa mwaka wa 2004, alipokuwa na umri wa miaka 19. Alifunga ndoa na Yevgeniya mwaka wa 2011.
Juni 12, 2018, maofisa wenye silaha na waliokuwa wameficha nyuso zao wa Idara ya Usalama wa Taifa (FSB) pamoja na askari, walivamia nyumba ya Feliks na Yevgeniya. Feliks alikamatwa na kuwekwa kizuizini kwa mwaka mmoja hivi. Aliimarishwa sana na sala alizotoa kwa ukawaida. Anasema hivi: “Kila siku nilisali kwa Yehova anipatie amani na shangwe kwa ajili ya siku hiyo.”
Septemba 19, 2019, Feliks na ndugu wengine watano walihukumiwa kifungo gerezani. Baada ya kushindwa rufaa yao, Feliks na ndugu wengine wanne, walihamishiwa katika gereza lililoko Orenburg, umbali wa kilomita 800 kutoka nyumba na familia zao katika jiji la Saratov. Walipofika, walipigwa vibaya sana.
Pamoja na hali zote hizo, Feliks amedumisha shangwe na tabasamu yake ambayo watu wengi wanaitambua. Yevgeniya anasema hivi: “Ninajivunia sana! Si tu kwamba alikuwa mtulivu mahakamani, bali pia anaendelea kuvumilia kwa utulivu na hata ananisaidia kuendelea kuvumilia.”
Ijapokuwa wenye mamlaka nchini Urusi walitaka kumdhuru Feliks na kuvunja imani yake, anasema kwamba mateso aliyopata yameimarisha ushikamanifu wake kwa Yehova. Jambo hilo linatukumbusha Mwanzo 50:20, Yosefu alipowaambia ndugu zake hivi: “Ingawa mlikusudia kunidhuru, Mungu alikusudia hali hiyo ibadilike na kuwa njema.”