Hamia kwenye habari

Kushota hadi kulia: Ndugu Konstantin Bazhenov, mke wake, Snezhana, na Dada Vera Zolotova

SEPTEMBA 21, 2020
URUSI

Ndugu Konstantin Bazhenov, Mke Wake, na Dada Mwenye Umri wa Miaka 73 Wanakabili Kifungo Nchini Urusi

Ndugu Konstantin Bazhenov, Mke Wake, na Dada Mwenye Umri wa Miaka 73 Wanakabili Kifungo Nchini Urusi

Siku Hukumu Itatangazwa

Septemba 25, 2020, a Mahakama ya Wilaya ya Yelizovsky katika Eneo la Kamchatka itatangaza uamuzi wake katika kesi kumhusu Ndugu Konstantin Bazhenov, mke wake, Snezhana, na Dada Vera Zolotova. Mwendesha-mashtaka ameomba Ndugu na Dada Bazhenov wapigwe faini ya rubo 600,000 (dola 7,850 za Marekani) na Dada Zolotova faini ya rubo 400,000 (dola 5,235 za Marekani).

Maelezo Mafupi Kuwahusu

Konstantin Bazhenov

  • Alizaliwa: 1977 (Petropavlovsk-Kamchatsky, Eneo la Kamchatka)

  • Maisha Yake: Ni mzaliwa wa kwanza katika familia yenye watoto wanne. Amefanya kazi akiwa fundi wa magari na amekuwa mwalimu katika shule ya ufundi. Anafurahia kuvua samaki

  • Mwaka wa 2001 alifunga ndoa na Snezhana, ambaye alikuwa pia mwalimu. Binti yao anaitwa Elizabeth. Familia yote inamtumikia Yehova

Snezhana Bazhenova

  • Alizaliwa: 1977 (Kisiwa cha Shikotan, Wilaya ya Sakhalin)

  • Maisha Yake: Alilelewa katika familia ya mzazi mmoja. Anawapenda watoto na alifurahia kufundisha katika shule ya msingi. Kwa sasa haruhusiwi kufanya kazi yoyote inayohusisha vijana kwa sababu ya mashtaka ya uhalifu dhidi yake

  • Alijifunza kumhusu Mungu na pia jinsi ya kusali kutoka kwa nyanya yake. Hilo lilimsaidia kupendezwa na mambo ya kiroho na kuipenda Biblia

Vera Zolotova

  • Alizaliwa: 1946 (Yelizovo, Eneo la Kamchatka)

  • Maisha Yake: Alilelewa katika familia kubwa. Mwaka wa 1966 alifunga ndoa na Yuri Zolotov. Wana watoto wawili. Ni mhasibu aliyestaafu. Anapenda kwenda matembezi na kuteleza kwenye barafu

  • Kwa miaka mingi alijaribu kujifunza kumhusu Mungu. Alichunguza dini nyingi tofauti. Hatimaye alifurahi kujifunza kwamba Mungu ni mwenye haki na anawapenda watu. Mume wake hakuwahi kuwa Shahidi wa Yehova. Hata hivyo, alivutiwa na jinsi Biblia ilivyoboresha maisha ya mke wake

Historia ya Kesi

Agosti 19, 2018, polisi walifanya msako katika nyumba tatu za Mashahidi katika mji wa Yelizovo. Jumla ya ndugu na dada 11 walikamatwa. Walihojiwa kwa saa nyingi. Mwishowe, Mashahidi wanane waliachiliwa. Lakini wenye mamlaka walifungua mashtaka dhidi ya Ndugu Bazhenov, mke wake, na Dada Zolotova na kuwaweka mahabusu. Baada ya siku mbili, akina dada waliachiliwa. Hakimu aliagiza kwamba Ndugu Bazhenov aendelee kukaa mahabusu. Aliachiliwa siku nane baadaye.

Tunasali kwamba Ndugu na Dada Bazhenov pamoja na Dada Zolotova wataendelea kumtegemea Yehova kikamili huku wakisubiri uamuzi wa kesi yao. Biblia inatuhakikisha kwamba Yehova atawajaza washikamanifu wake shangwe na amani, na kwamba ‘tumaini lao litaongezeka kwa nguvu za roho takatifu.’—Waroma 15:13.

a Huenda itabadilika