Hamia kwenye habari

Ndugu Konstantin Guzev

FEBRUARI 19, 2021
URUSI

Ndugu Konstantin Guzev Ahukumiwa kwa Sababu ya Imani Yake

Ndugu Konstantin Guzev Ahukumiwa kwa Sababu ya Imani Yake

HABARI ZA KARIBUNI | Ndugu Konstantin Guzev Ameshindwa Rufaa Yake

Mei 13, 2021, Mahakama ya Eneo Lililotengewa Wayahudi imekataa rufaa ya Ndugu Guzev. Hukumu yake ya awali ya kifungo cha nje cha miaka miwili na miezi sita itaanza kutumika. Hatahitaji kwenda gerezani wakati huu.

Hukumu

Februari 18, 2021, Mahakama ya Wilaya ya Birobidzhan katika Eneo Lililotengewa Wayahudi ilimhukumu Ndugu Konstantin Guzev kifungo cha nje cha miaka miwili na nusu. Hatahitaji kwenda gerezani wakati huu.

Maelezo Mafupi Kumhusu

Konstantin Guzev

  • Alizaliwa: 1964 (Khabarovsk)

  • Maisha Yake: Baba yake alikuwa mtu mwenye jeuri na mlevi. Alijiuliza ikiwa maisha yana kusudi. Alipokosa kupata majibu, alianza kutumia dawa za kulevya na kileo. Hatimaye, alianza kujifunza Biblia na Mashahidi wa Yehova. Alipata majibu yenye kuridhisha ya maswali yake. Alifanya mabadiliko makubwa katika maisha yake. Alibatizwa katika mwaka wa 2000. Alifunga ndoa na Anastasiya mwaka wa 2001

Historia ya Kesi

Wenye mamlaka walipekua nyumba ya Konstantin mnamo Mei 2018 wakati wa msako ulioitwa “Siku ya Hukumu.” Wakati wa msako huo, maofisa wa usalama walipekua nyumba katika jiji lote la Birobidzhan. Julai 29, 2019, wenye mamlaka walifungua kesi ya uhalifu dhidi ya Konstantin. Alishtakiwa kwa “kupanga utendaji wa shirika lenye msimamo mkali” kwa sababu tu aliongoza mikutano ya kidini.

Kesi 19 tofauti zimefunguliwa dhidi ya Mashahidi 22 wa Yehova katika eneo hilo. Anastasiya, mke wa Konstantin, pia amefunguliwa kesi moja.

Mfano wa ujasiri uliowekwa na ndugu na dada wengine nchini Urusi umewaimarisha Konstantin na Anastasiya. Konstantin anasema hivi: “Nimejionea kwa macho yangu na kusikia kwa masikio yangu mwenyewe akina dada fulani mwanzoni wakisema hawatazungumza kabisa mahakamani. . . . Lakini kwa msaada wa Yehova na kupitia sala za akina ndugu, walizungumza kwa njia nzuri na kutetea imani yao.”

Tunaendelea kusali na kuwafikiria ndugu na dada wote nchini Urusi. Tuna uhakika kwamba hakuna mpango uliofanywa dhidi yao utakaofanikiwa kuvunja imani yao kwa sababu Yehova yuko pamoja nao.—Isaya 8:10.