Hamia kwenye habari

Ndugu Dmitriy Mikhaylov alipohojiwa hivi karibuni. Alikamatwa na wenye mamlaka nchini Urusi Mei 29, 2018, na kuwekwa mahabusu siku 171

JUNI 18, 2019
URUSI

Ndugu Mikhaylov Aliwekwa Mahabusu Kinyume cha Sheria—Umoja wa Mataifa

Ndugu Mikhaylov Aliwekwa Mahabusu Kinyume cha Sheria—Umoja wa Mataifa

Jopo la wataalamu wa nchi kadhaa la Umoja wa Mataifa (UM) limesema kwamba kukamatwa kwa Ndugu Dmitriy Mikhaylov na kuwekwa mahabusu na nchi ya Urusi ni “ubaguzi kwa msingi wa kidini” na hivyo kulipinga sheria za kimataifa. Pia jopo hilo lilihimiza nchi ya Urusi imwondolee mashtaka yote.

Kulingana na maoni ya kurasa 12 yaliyotolewa na jopo hilo, Kamati ya Umoja wa Mataifa Inayoshughulikia Vifungo Visivyo vya Haki (WGAD), matendo ya Ndugu Mikhaylov “sikuzote yamekuwa ya amani.” Pia, “hakuna uthibitisho kwamba yeye au Mashahidi wa Yehova nchini Urusi wameshiriki jeuri au kuwachochea wengine washiriki jeuri.”

WGAD ilimalizia kwa kusema kwamba Ndugu Mikhaylov “alitumia haki yake tu ya uhuru wa kidini” na “hakupaswa kukamatwa na kuwekwa mahabusu.” Hivyo, anastahili kulipwa kwa kukosa mshahara na pia kwa kupoteza uhuru alipowekwa mahabusu kinyume cha sheria.

WGAD pia ilitambua kwamba si Ndugu Mikhaylov peke yake anayevumilia ukosefu wa haki kwa sababu ya imani yake. Yeye “peke yake ndiye mmoja kati ya idadi inayoongezeka ya Mashahidi wa Yehova nchini Urusi aliyeshtakiwa kushiriki uhalifu kwa msingi wa kutekeleza uhuru wake wa kidini”—haki ambayo inalindwa na sheria ya kimataifa. Hivyo, WGAD ilijitahidi kushutumu mateso yanayowapata waabudu wenzetu nchini Urusi kwa kusema kwamba maoni waliyotoa hayamhusu Ndugu Mikhaylov peke yake bali Mashahidi wote wa Yehova walio “katika hali kama za Bw. Mikhaylov.”

Ndugu Mikhaylov alianza kujifunza Biblia akiwa tineja na akabatizwa mwaka wa 1993, alipokuwa na umri wa miaka 16. Mwaka wa 2003, alimwoa Yelena, na wakaanza kumtumikia Yehova pamoja.

Mwaka wa 2018, Ndugu na Dada Mikhaylov waligundua kwamba wenye mamlaka walikuwa wakirekodi mazungumzo katika simu zao na walikuwa wamechukua video za kuwachunguza kwa miezi kadhaa. Aprili 19, 2018, Kamati ya Uchunguzi ya nchi ya Urusi katika eneo la Ivanovo ilifungua kesi ya uhalifu dhidi ya Ndugu Mikhaylov na maofisa wenye silaha walikuja kupekua nyumba yake. Mwezi mmoja hivi baadaye, alikamatwa na kuwekwa mahabusu, kwa madai ya kuchangia kifedha utendaji “wenye msimamo mkali.” Baada ya kuwekwa mahabusu kwa karibu miezi sita, yaani, siku 171, aliachiliwa. Hata hivyo, haruhusiwi kusafiri na mawasiliano yake yamedhibitiwa hadi wenye mamlaka watakapofunga kesi yake ya uhalifu.

Serikali ya Urusi imepewa miezi sita kutekeleza maoni ya WGAD, katika muda huo inapaswa kusema ikiwa kesi ya uhalifu dhidi ya Mikhaylov imefungwa, ikiwa amerudishiwa gharama za kesi, na ikiwa waliovunja haki zake wamefanyiwa uchunguzi.

Inawezekana kwamba maoni kama hayo ya WGAD yalibadili jinsi Ndugu Teymur Akhmedov anayeishi Kazakhstan alivyotendewa. Mwaka wa 2017, alikamatwa na kuhukumiwa kifungo cha miaka mitano kwa kushiriki imani yake kwa amani pamoja na wengine. Baada ya kuchukua hatua zote za kisheria nchini humo, mawakili wa Ndugu Akhmedov walituma malalamiko kwa WGAD. Katika maoni yao yaliyotolewa Oktoba 2, 2017, WGAD ilishutumu matendo ya wenye mamlaka nchini Kazakhstan na kusema kwamba Ndugu Akhmedov anapaswa kuachiliwa. Miezi sita baadaye, rais wa Kazakhstan alimsamehe Ndugu Akhmedov. Aliachiliwa Aprili 4, 2018.

Hata iwe nchi ya Urusi itatendaje kufuatia uamuzi wa WGAD katika kisa cha Ndugu Mikhaylov, tuna uhakika kabisa kuhusu ahadi hii: “Mwenye furaha ni mtu anayemkimbilia [Yehova].” Tunasali kwamba Yehova aendelee kuwatunza ndugu na dada zetu nchini Urusi ambao wanakabili mashtaka ya uhalifu, ili waendelee kujionea kwamba wote wanaomtumaini kwa ujasiri “hawatakosa chochote chema.”—Zaburi 34:8, 10.