Hamia kwenye habari

Ndugu Sergey Ledenyov na mke wake, Anna

NOVEMBA 20, 2020
URUSI

Ndugu Sergey Ledenyov Anakabili Kifungo cha Miaka Sita Gerezani Nchini Urusi

Ndugu Sergey Ledenyov Anakabili Kifungo cha Miaka Sita Gerezani Nchini Urusi

Hukumu Inatarajiwa

Novemba 24, 2020, a Mahakama ya Jiji la Petropavlovsk-Kamchatskiy katika Eneo la Kamchatka inatarajiwa kutangaza uamuzi katika kesi dhidi ya Ndugu Sergey Ledenyov. Anakabili miaka sita gerezani.

Maelezo Mafupi Kumhusu

Sergey Ledenyov

  • Alizaliwa: 1974 (Ossora, Eneo la Kamchatka)

  • Maisha Yake: Alizaliwa katika familia yenye watoto sita. Anapenda kuchora na kupiga picha. Anafanya kazi akiwa mjenzi na kuweka vigae. Zamani aliona Biblia kuwa kitabu ambacho hakipatani na sayansi na kilichopitwa na wakati hadi alipojifunza pamoja na Mashahidi wa Yehova. Mwaka wa 2017, alifunga ndoa na Anna. Mke wake Anna anasema kwamba kutumia kanuni za Biblia kumemfanya Sergey awe mume mtulivu, anayejali, na mwenye upendo.

Historia ya Kesi

Desemba 2, 2018, kikundi cha maofisa waliobeba silaha na waliofunika nyuso zao walishambulia nyumba ya Ndugu Ledenyov huko Petropavlovsk-Kamchatskiy. Aliwekwa kizuizini na kushtakiwa chini ya Kifungu 282.2 cha Sheria ya Uhalifu ya Urusi. Kesi ya uhalifu ilianza Novemba 28, 2019.

Desemba 12, 2019, Mahakama ya Jiji la Petropavlovsk-Kamchatskiy katika Eneo la Kamchatka ilirudisha kesi hiyo kwenye ofisi ya mwendesha-mashtaka. Jambo kama hilo hutokea tu wakati ambapo mahakama inagundua kasoro kubwa katika mashtaka, kama vile ukosefu wa ushahidi. Hata hivyo, Februari 4, 2020, mahakama kuu ilibadili uamuzi huo na kuendelea na kesi hiyo. Baadaye, kesi hiyo iliposikilizwa, wenye mamlaka walimhoji mke wa Ndugu Ledenyov na dada mwingine na wakajaribu kuwalazimisha waseme uwongo dhidi ya Ndugu Ledenyov. Dada Ledenyov na dada yule mwingine walikataa kabisa kufanya hivyo.

Watu wa ukoo wa Ndugu Ledenyov ambao si Mashahidi hawaelewi kwa nini anateswa kwa sababu ya imani yake.

Tunaendelea kusali kwa ajili ya Ndugu na Dada Ledenyov wanaposubiri uamuzi wa kesi hiyo. Tuna uhakika kwamba roho ya Yehova inaendelea kutulia kabisa juu yao.—1 Petro 4:14.

a Inaweza kubadilika.