Hamia kwenye habari

Ndugu Andrey Stupnikov (katikati), pamoja na marafiki, baada ya uamuzi wa mahakama wa kumwachia huru kutoka katika kifungo cha nyumbani

JULAI 5, 2019
URUSI

Ndugu Stupnikov Aachiliwa Huru Baada ya Kifungo cha Nyumbani

Ndugu Stupnikov Aachiliwa Huru Baada ya Kifungo cha Nyumbani

Julai 2, 2019, mahakama ya Krasnoyarsk, Urusi, ilitoa uamuzi wa kumwachilia huru Ndugu Andrey Stupnikov aliyekuwa katika kifungo cha nyumbani. Ijapokuwa hayupo chini ya kifungo hicho kwa sasa, bado kesi yake ya uhalifu iko wazi.

Ndugu Andrey Stupnikov

Alfajiri ya Julai 3, 2018, familia ya Stupnikov ilikuwa ipande ndege katika Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Krasnoyarsk. Maafisa wawili wa Usalama wa Taifa waliwafuata na kumkamata Ndugu Stupnikov. Akawekwa mahabusu kwa muda wa miezi minane kabla ya kuhamishiwa kwenye kifungo cha nyumbani mwishoni mwa Februari 2019.

Ndugu Stupnikov anahisi kwamba amejifunza mengi kujihusu na kuhusu uhusiano wake na Yehova kwa kipindi cha mwaka mmoja uliopita. Anasema: “[Mimi na Olga] tumekuwa Mashahidi kwa miaka mingi lakini hatukuwahi kuwa na uhusiano wa karibu na Yehova kama sasa! Katika hali ngumu zaidi nilihisi na ninaendelea kuhisi kwamba Baba yetu ni halisi zaidi maishani mwetu na yeye hutusaidia. Ninaguswa moyo sana kujua jinsi Yehova yuko karibu nami na jinsi alivyojibu sala zangu kwa uharaka!”

Ndugu Stupnikov anamalizia kwa kusema: “Sasa kuliko wakati mwingine wowote, nina uhakika kwamba Baba yangu ananijua na anaelewa hisia zangu. Mambo niliyojionea mwenyewe yamenisaidia kumtegemea Yehova kikamili na kutokuwa na wasiwasi sana kuhusu mateso. Jambo la kuogopesha zaidi ni kupoteza uhusiano huo wa karibu na Yehova. Nina uhakika kwamba nikiwa pamoja naye ninaweza kukabiliana na kitu chochote.”

Kufikia Julai 1 idadi inayoongezeka ya kesi za uhalifu dhidi ya ndugu na dada zetu nchini Urusi imefikia 217. Kwa mara kadhaa, maofisa wa serikali nchini Urusi wamewapunguzia vizuizi ndugu na dada zetu. Ingawa hivyo, hatuweki tegemeo letu katika mahakama za kibinadamu au wakuu wa serikali lakini tunaendelea kumtegemea Yehova. Tunasali kwamba Yehova aendelee kuwapa nguvu na kuwalinda waabudu wenzetu nchini Urusi.—Zaburi 28:7.