Hamia kwenye habari

Juu kuanzia kushoto: Ndugu Andrey Tabakov, Ndugu Mikhail Zelenskiy, Ndugu na Dada Mysin. Chini kuanzia kushoto: Ndugu Khoren Khachikyan na Ndugu Aleksandr Ganin

OKTOBA 2, 2020
URUSI

Ndugu Wanne na Wenzi wa Ndoa Wanakabili Kifungo cha Miaka Saba Nchini Urusi

Ndugu Wanne na Wenzi wa Ndoa Wanakabili Kifungo cha Miaka Saba Nchini Urusi

Siku Hukumu Itatangazwa

Oktoba 5, 2020, a the Mahakama ya Wilaya ya Zasviyazhsky katika Jiji la Ulyanovsk inakusudia kutangaza uamuzi wake katika kesi inayohusu Ndugu Aleksandr Ganin, Khoren Khachikyan, Andrey Tabakov, na Mikhail Zelenskiy, kutia ndani Ndugu Sergey Mysin na mke wake, Nataliya. Wote wanakabili vifungo mbalimbali, kuanzia miaka mitatu hadi miaka saba. Pia, mwendesha-mashtaka ameiomba mahakama iwanyang’anye pesa na magari yao—jumla ya rubo milioni 1.57 (dola 20,000 za Marekani).

Maelezo Mafupi Kuwahusu

Aleksandr Ganin

  • Alizaliwa: 1957 (Ekhabi, Kisiwa cha Sakhalin)

  • Maisha Yake: Alibatizwa zaidi ya miaka 20 iliyopita na kuwa Shahidi wa Yehova. Sasa amestaafu na anapenda kutunza bustani

Khoren Khachikyan

  • Alizaliwa: 1985 (Yerevan, Armenia)

  • Maisha Yake: Ana shahada katika uchumi. Alikuwa mcheza-mweleka alipokuwa kijana. Anajulikana kuwa mwanamume mpole na mwenye fadhili

  • Alianza kujifunza Biblia na Mashahidi wa Yehova kwa sababu alitaka kumjua Mungu vizuri zaidi na kuishi kulingana na amri zake. Anaipenda Biblia kwa sababu inaelezea mambo yanayopatana na akili na haijipingi yenyewe.

Sergey Mysin

  • Alizaliwa: 1965 (Kulebaki, Eneo la Nizhny Novgorod)

  • Maisha Yake: Alikutana na mke wake, Nataliya, alipokuwa akisomea kuwa injinia. Walifunga ndoa mwaka wa 1991. Wamekuwa wakimtumikia Yehova pamoja kwa zaidi ya miaka 20 na wana watoto wawili wenye umri mkubwa. Anafurahia michezo, hasa mchezo wa lacrosse

Nataliya Mysina

  • Alizaliwa: 1971 (Leningrad, sasa inajulikana Saint Petersburg)

  • Maisha Yake: Alizaliwa katika familia ya wanajeshi. Aliishi Ujerumani alipokuwa chuo akisomea kuwa mfamasia. Anapenda kupika na kuoka

Andrey Tabakov

  • Alizaliwa: 1973 (Minsk, Belarus)

  • Maisha Yake: Anafanya kazi katika taaluma ya teknolojia ya mawasiliano. Mwaka wa 2006 alimwoa Marina. Walijifunza Biblia na Mashahidi wa Yehova na kubatizwa. Anapenda kurekebisha vifaa vya kielektroni, hasa redio na kompyuta

Mikhail Zelenskiy

  • Alizaliwa: 1960 (Bulaesti, Moldova)

  • Maisha Yake: Amefanya kazi akiwa baharia na mwendesha malori. Mnamo 1989, alimwoa Victoria. Mapema katika miaka ya 1990, alianza kujifunza Biblia. Hatua kwa hatua upendo wao kwa Yehova uliongezeka na wakabatizwa

Historia ya Kesi

Karibu miaka mitatu iliyopita, maofisa wa Idara ya Usalama wa Taifa (FSB) walianzisha oparesheni ya kuwachunguza ndugu na dada zetu katika eneo la Ulyanovsk, iliyotia ndani kurekodi mazungumzo yao ya simu. Februari 24, 2019, FSB ilianzisha uchunguzi dhidi ya Ndugu na Dada Mysin, Ndugu Khachikyan, Ndugu Tabakov, na Ndugu Zelenskiy.

Siku tatu baadaye, saa 11 alfajiri, maofisa walivamia nyumba za Ndugu Khachikyan, Ndugu Tabakov, na Ndugu Zelenskiy. Ndugu hao watatu walikamatwa na kuzuiliwa kwa muda. Asubuhi hiyo, Dada Mysina alipigiwa simu. Aliambiwa kwamba gari lao lilikuwa limeharibiwa na hivyo yeye na mume wake Sergey wanahitaji kutoka nje. Mara tu Ndugu Mysin alipofungua mlango, maofisa wa FSB waliingia kwa kishindo ndani ya nyumba yao. Maofisa hao walipekua nyumba hiyo na kuchukua vifaa vya kielektroni vya familia hiyo. Kisha wenzi hao wa ndoa walikamatwa.

Siku iliyofuata, Mahakama ya Wilaya ya Leninsky katika Eneo la Ulyanovsk iliamuru Ndugu Mysin awekwe mahabusu. Dada Mysina na ndugu wale wengine watatu walipewa kifungo cha nyumbani.

Ndugu Mysin alikaa mahabusu jumla ya siku 55 na siku 123 katika kifungo cha nyumbani. Dada Mysina, Ndugu Khachikyan, Ndugu Tabakov, na Ndugu Zelenskiy waliwekwa katika kifungo cha nyumbani kwa siku 50 hadi 55.

Asubuhi ya Mei 15, 2019, maofisa wa FSB walipekua nyumba ya Ndugu Ganin na kumkamata. Alifungwa kwa siku mbili katika gereza la kuzuilia watu kwa muda.

Wahubiri wote sita wamewekewa vizuizi vya kadiri. Hata hivyo, wenye mamlaka wanaendelea kuwashinikiza katika njia nyingine. Wenye mamlaka wamewazuia Ndugu na Dada Mysin wasitumie rubo 500,000 (dola 6,313 za Marekani) zilizo katika akaunti yao ya benki. Pia, wamemzuia Ndugu Tabakov asitumie rubo 600,000 (dola 7,575 za Marekani) zilizo katika akaunti yake ya benki.

Tunasali kwamba maneno haya ya mtunga-zaburi yaliyoongozwa na roho yaendelee kuwaimarisha ndugu na dada zetu nchini Urusi wanaoteswa kwa sababu ya imani yao: “Mungu ni kimbilio letu na nguvu zetu, msaada unaopatikana kwa urahisi nyakati za taabu.”—Zaburi 46:1.

[Maelezo ya chini]

a Inaweza kubadilishwa