Septemba 1, 2021
URUSI
Ndugu Wawili Wagonjwa Sana Waachiliwa Kutoka Mahabusu Baada ya Ombi la ECHR
Agosti 28, 2021, Ndugu Aleksandr Lubin na Anatoliy Isakov waliachiliwa kutoka mahabusu baada ya Mahakama ya Ulaya ya Haki za Kibinadamu (ECHR) kutoa ombi kwa wenye mamlaka nchini Urusi. Hata ingawa ndugu hao ni walemavu, walizuiliwa kwa mwezi mmoja na nusu katika Eneo la Kurgan la Urusi. Wanaweza kufungwa gerezani kwa kuwa bado wanasubiri matokeo ya kesi yao ya uhalifu.
Julai 13 na 14, 2021, maofisa wa usalama katika Eneo la Kurgan walivamia nyumba za Mashahidi wa Yehova. Ndugu Isakov, ambaye ana umri wa miaka 56, na Ndugu Lubin, aliye na umri wa miaka 65, walikuwa baadhi ya Mashahidi waliopelekwa kizuizini.
Ndugu Lubin ana tatizo kubwa la mfumo wa damu, kupanda kwa shinikizo la damu, na ugonjwa wa mfumo wa kinga unaoathiri viungo vyake. Anahitaji kuwekwa kwenye mashine ya oksijeni kwa saa 16 kila siku na kupata matibabu mengine, ambayo hakuruhusiwa kupata. Ana matatizo ya kutembea na hawezi kujiinua bila msaada. Tatyana, mke wake ni mlemavu pia na amepatwa na kiharusi mara nne.
Ndugu Isakov aligunduliwa kuwa na kansa ya damu na baadhi ya mifupa yake ya mgongo na mbavu imevunjika hivi kwamba anahitaji kutumia gari la magurudumu. Hakuruhusiwa kupata matibabu yake ya mionzi alipokuwa kizuizini. Pia hakuruhusiwa kupata dawa zake za maumivu. Kwa kusikitisha, Ndugu Isakov aliambukizwa COVID-19 alipokuwa mahabusu.
Kwa majuma mengi, mawakili walikata rufaa mahakamani ili ndugu hao wawili waachiliwe kutoka mahabusu lakini hawakufanikiwa. Badala yake, mahakimu walifanya maamuzi yao kwa kutegemea hati za madaktari kwenye Hospitali ya Eneo la Kurgan ambao kwa kustaajabisha walisema Ndugu Lubin na Ndugu Isakov hawakuwa na magonjwa yaliyowazuia kuwekwa mahabusu.
Agosti 8, 2021, mawakili waliwasilisha malalamishi kwenye ECHR. Mahakama hiyo ikatuma ombi kwenye Ofisi ya Mwendesha-Mashtaka Mkuu wa Shirikisho la Urusi. Agosti 24, 2021, ndugu hao wawili walipelekwa tena kwenye Hospitali ya Eneo la Kurgan. Pindi hii madaktari wakasema kwamba Ndugu Lubin na Ndugu Isakov walikuwa na magonjwa ambayo yaliwazuia kuwekwa mahabusu.
Tunasali kwa ajili ya ndugu hao wawili ambao wanadumisha utimilifu wao licha ya mateso na magonjwa. Tunajua kwamba Yehova ataendelea ‘kudhihirisha nguvu zake’ kwa niaba yao.—2 Mambo ya Nyakati 16:9.