Hamia kwenye habari

Kushoto hadi kulia: Ndugu Vladimir Khokhlov, Dada Tatyana Shamsheva, Dada Olga Silaeva, na Ndugu Eduard Zhinzhikov

SEPTEMBA 3, 2020
URUSI

Ndugu Wawili na Dada Wawili Wamehukumiwa kwa Sababu ya Imani Yao

Ndugu Wawili na Dada Wawili Wamehukumiwa kwa Sababu ya Imani Yao

Hukumu

Septemba 3, 2020, Mahakama ya Mji wa Novozybkov katika eneo la Bryansk ilihukumu Ndugu Vladimir Khokhlov, Dada Tatyana Shamsheva, Dada Olga Silaeva, na Ndugu Eduard Zhinzhikov vifungo vya mwaka mmoja hadi mwaka mmoja na miezi mitatu gerezani. Hata hivyo, kwa kuwa tayari walikuwa wametumikia vifungo vyao mahabusu, waliachiliwa.

Maelezo Mafupi Kuwahusu

Vladimir Khokhlov

  • Tarehe ya Kuzaliwa: 1977 (Novozybkov, Eneo la Bryansk)

  • Maisha Yake: Anafanya kazi ya kurekebisha magari. Alitumikia jeshini kabla yakuwa Shahidi wa Yehova. Anapenda kucheza mpira, kusoma, kuvua samaki, na kucheza gitaa

  • Rafiki yake alimtia moyo kujifunza Biblia. Alifunga ndoa na Olga mnamo 2007. Wana binti mmoja anayeitwa Anastasia. Familia nzima inamtumikia Yehova pamoja

Tatyana Shamsheva

  • Tarehe ya Kuzaliwa: 1977 (Cherepovets, Eneo la Vologda)

  • Maisha Yake: Ni mtaalamu wa uchumi. Amefundisha somo la uchumi, sheria, na uhasibu kwa miaka mingi. Alibatizwa mwaka wa 1995. Anafurahia kuwaonyesha wengine mashauri yenye hekima yaliyo katika Biblia

Olga Silaeva

  • Tarehe ya Kuzaliwa: 1988 (Davydovo, Eneo la Moscow)

  • Maisha Yake: Ndiye mtoto wa mwisho kati ya watoto watatu. Amehitimu chuo cha ufundi. Anapenda kushona. Anapenda kusoma na kucheza mpira wa wavu. Alifuata mfano wa mama yake akajifunza Biblia na kukubali mafundisho ya Biblia

Eduard Zhinzhikov

  • Tarehe ya Kuzaliwa: 1971 (Zadnya, Eneo la Bryansk)

  • Maisha Yake: Amefanya kazi ya kuchomelea vyuma na ya kusafisha majengo, na amewahi kuajiriwa na polisi. Alikuwa katika bendi ya muziki. Mnamo 1993, alifunga ndoa na Tatyana, aliyekuwa mshiriki mwenzake wa bendi. Anapenda kuandika mashairi na kupiga gitaa

  • Muda mfupi kabla ya mwaka wa 2000, alianza kujifunza Biblia na akapata majibu ya maswali yake mengi. Majibu hayo yalimfanya abadili mazoea yake mabaya na kuboresha maisha ya familia yake. Tatyana alivutiwa na hilo. Kwa hiyo, akaamua kuwa Shahidi pia

Historia ya Kesi

Juni 11, 2019, wenye mamlaka walivamia nyumba 22 za Mashahidi katika Eneo la Bryansk nchini Urusi. Dada Tatyana Shamsheva na Dada Olga Silaeva walikamatwa. Kila mmoja wao aliwekwa mahabusu kwa siku 245. Waliachiliwa mnamo Mei 2020 na wakarudi nyumbani ili kusubiri kusikilizwa kwa kesi yao.

Oktoba 16, 2019, wenye mamlaka walifungua mashtaka ya uhalifu dhidi ya Ndugu Vladimir Khokhlov na Ndugu Eduard Zhinzhikov. Baadaye, kesi yao iliunganishwa na kesi ya Dada Shamsheva na Dada Silaeva. Siku saba baadaye, ndugu hao waliwekwa mahabusu, na bado wako huko mpaka leo.

Dada hao walihojiwa katika Ripoti ya 5 ya Baraza Linaloongoza ya 2020. Dada Silaeva alisema kwamba kukaa mahabusu miezi nane kulimhakikishia kwamba “hata hali ziwe ngumu kadiri gani, sikuzote Yehova atanipatia roho takatifu, ili kukabiliana na jaribu lolote ambalo nitakabili.” Dada Shamsheva alisema hivi kwa uhakika: “Yehova yuko karibu nasi, sikuzote yeye hututegemeza, hutuimarisha, na kutusaidia.”

Tuna uhakika kwamba Yehova ataendelea kuwasaidia ndugu na dada zetu wote nchini Urusi ambao wanakabili kifungo au ambao tayari wamefungwa, wavumilie majaribu yao kwa shangwe na amani.—1 Wakorintho 10:13.