Hamia kwenye habari

Kutoka kushoto hadi kulia: Aleksey Budenchuk, Konstantin Bazhenov, Feliks Makhammadiyev, Aleksey Miretskiy, Roman Gridasov, na Gennadiy German, kabla ya kukamatwa

SEPTEMBA 23, 2019
URUSI

Ndugu Wengine Sita Wamehukumiwa na Kufungwa Nchini Urusi

Ndugu Wengine Sita Wamehukumiwa na Kufungwa Nchini Urusi

Alhamisi, Septemba 19, 2019, ndugu sita wanaoishi kwenye jiji la Saratovi, nchini Urusi, walihukumiwa kufungwa gerezani kwa sababu tu wao ni Mashahidi wa Yehova.

Hakimu Dmitry Larin wa Mahakama ya Wilaya ya Leninsky iliyoko Saratov alimhukumu Ndugu Konstantin Bazhenov na Ndugu Aleksey Budenchuk miaka mitatu na miezi sita gerezani; Ndugu Feliks Makhammadiyev alihukumiwa miaka mitatu gerezani; Ndugu Roman Gridasov, Ndugu Gennadiy German, na Ndugu Aleksey Miretskiy walihukumiwa miaka miwili gerezani. Isitoshe, uamuzi wa mahakama unasema kwamba baada ya kukamilisha kifungo chao, ndugu wote hao watapigwa marufuku wasitumikie katika vyeo vya usimamizi katika shirika lolote la umma kwa kipindi cha miaka mitano. Upande wa utetezi unapanga kukata rufaa ili kupinga uamuzi huo.

Mashtaka ya uhalifu yalitolewa kwa mara ya kwanza dhidi ya ndugu hao sita baada ya wenye mamlaka wa Urusi kuvamia nyumba saba za Mashahidi jijini Saratov Juni 12, 2018. Ndugu wote hao wana familia, lakini Ndugu Budenchuk ana watoto wawili ambao bado wako shuleni. Ndugu Budenchuk, pamoja na Ndugu Bazhenov na Ndugu Makhammadiyev, walizuiliwa kwa karibu mwaka mmoja wakisubiri kesi yao kusikilizwa.

Katika maneno yao ya mwisho mbele ya mahakama, ndugu wote sita walinukuu mistari kadhaa yenye kuchochea kutoka katika Biblia na kusema kwamba hawakuwa na chuki yoyote dhidi ya waendesha-mashtaka.

Sasa Urusi imewahukumu na kuwafunga akina ndugu saba. Zaidi ya akina ndugu na dada 250 nchini Urusi wameshtakiwa kwa uhalifu, 41 kati yao wakiwa wamezuiliwa (iwe wanasubiri kesi isikilizwe au wako gerezani) na wengine 23 wako katika kifungo cha nyumbani.

Tunasali kwa ajili ya ndugu na dada wote waaminifu na wenye ujasiri nchini Urusi kwamba ‘waimarishwe kwa nguvu zote kwa uwezo wa Yehova wenye utukufu ili wavumilie kikamili kwa subira na shangwe.’—Wakolosai 1:11.