Hamia kwenye habari

Agosti 26, 2020, Ndugu Yuriy Savelyev akiwa kizimbani mahakamani

DESEMBA 11, 2020
URUSI

Ndugu Yuriy Savelyev, Amezuiliwa kwa Zaidi ya Miaka Miwili, Anaweza Kufungwa Miaka Nane Gerezani

Ndugu Yuriy Savelyev, Amezuiliwa kwa Zaidi ya Miaka Miwili, Anaweza Kufungwa Miaka Nane Gerezani

Hukumu Inatarajiwa

Desemba 16, 2020, a Mahakama ya Wilaya ya Leninskiy iliyoko Novosibirsk inatarajiwa kutangaza uamuzi katika kesi inayomhusu Ndugu Yuriy Savelyev. Mwendesha-mashtaka aliomba Yuriy afungwe miaka minane gerezani. Ikiwa mahakama itakubali, hicho kitakuwa ndicho kifungo kirefu zaidi ambacho yeyote kati ya ndugu zetu nchini Urusi amepewa tangu uamuzi wa Mahakama Kuu wa mwaka 2017.

Maelezo Mafupi Kumhusu

Yuriy Savelyev

  • Alizaliwa: 1954 (Krokhalyovka, Eneo la Novosibirsk)

  • Maisha Yake: Mama yake alikufa alipokuwa mtoto mchanga. Alilelewa na dada yake. Alifanya kazi akiwa fundi-bomba katika kiwanda cha kuzalisha nishati. Alipendezwa na dini baada ya kifo cha mke wake. Alitambua kwamba Biblia inamsaidia kupata majibu yanayopatana na akili ya maswali yake. Alibatizwa na kuwa Shahidi wa Yehova mwaka wa 1996

Historia ya Kesi

Novemba 8, 2018, polisi walivamia nyumba yake pamoja na nyumba nyingine tisa za Mashahidi katika Eneo la Novosibirsk. Yuriy alikamatwa na kuwekwa mahabusu.

Yuriy alishtakiwa kwa kupanga utendaji wa Mashahidi wa Yehova katika jiji lao. Muda wake wa kukaa mahabusu uliongezwa mara tisa licha ya kukata rufaa mara nyingi kwamba aachiliwe. Amekaa kifungoni kwa zaidi ya miaka miwili. Tangu uamuzi wa Mahakama Kuu ya Urusi uliotolewa mwaka wa 2017, ni Ndugu Dennis Christensen na Ndugu Sergey Klimov ambao wamekaa kwa muda mrefu zaidi gerezani kuliko Ndugu Savelyev.

Jumatano, Desemba 9, 2020, Yuriy alipokuwa akitoa maelezo yake ya kumalizia mahakamani, alimwambia hakimu hivi kwa ujasiri: “Nimejikuta nikishtakiwa, si kwa sababu ya uhalifu, bali kwa sababu ya kufuata mafundisho ya kidini ya Mashahidi wa Yehova.

“Sina maadui, na tangu nilipozaliwa miaka 67 iliyopita sijawahi kushtakiwa kwa uhalifu. Nimeamua kwamba sitaunga mkono upande wowote katika mambo ya kisiasa. Ninamaanisha kwamba ninapinga jeuri ya aina zote, iwe ni kwa maneno, kisaikolojia, au kimwili.

“Sheria ya Mungu inadai niwatendee watu wote kwa heshima, bila kujali wao ni nani katika jamii, taifa lao, au imani yao ya kidini.

“Pia, Neno la Mungu linatuhimiza tuwatendee wenye mamlaka wa heshima. Barua ya Waroma 13:1-3, inasema hivi kwa sehemu: ‘Kila mtu na ajitiishe kwa mamlaka zilizo kubwa, kwa maana hakuna mamlaka isipokuwa kupitia Mungu; mamlaka zilizopo zimewekwa na Mungu katika vyeo vyao vya kadiri. Kwa hiyo, yeyote anayepinga mamlaka amechukua msimamo dhidi ya mpango wa Mungu.’

“Mimi sipingi mamlaka, kwa sababu sitaki kuchukua msimamo dhidi ya Mungu. Mungu huwaangamiza wote wanaompinga. Mashahidi wa Yehova ndio walionisaidia kumjua Mungu wa pekee wa kweli na mwana wake, Yesu Kristo. Walinisaidia pia kusadiki kwamba Maandiko Matakatifu, Biblia, ni kitabu cha pekee. Inatusaidia katika sehemu zote za maisha yetu.”

Tunatiwa moyo kusikia kwamba imani ya Yuriy ni yenye nguvu, na kuona kwamba Yehova anaendelea kumbariki kwa amani inayodumu.​—Isaya 26:3.

a Inaweza kubadilishwa.