Hamia kwenye habari

SEPTEMBA 23, 2020
URUSI

Ndugu Yuriy Zalipayev Anakabili Kifungo cha Miaka Miwili Gerezani Nchini Urusi

Ndugu Yuriy Zalipayev Anakabili Kifungo cha Miaka Miwili Gerezani Nchini Urusi

Siku Hukumu Itatangazwa

Oktoba 7, 2020, a Mahakama ya Wilaya ya Mayskiy ya Jamhuri ya Kabardino-Balkaria inakusudia kutangaza uamuzi wake katika kesi kumhusu Ndugu Yuriy Zalipayev. Anakabili kifungo cha miaka miwili gerezani.

Maelezo Mafupi Kumhusu

Yuriy Zalipayev

  • Alizaliwa: 1962 (Samara)

  • Maisha Yake: Amefanya kazi ya kuchomelea vyuma na kuendesha lori. Anapenda mashairi na kwenda matembezi

  • Katika mwaka wa 1983 alifunga ndoa na Natalia, aliyekuwa mwanafunzi mwenzake walipokuwa watoto. Miaka kumi baadaye, walianza kujifunza Biblia pamoja. Wana watoto watatu. Wote wanamtumikia Yehova pamoja na watu fulani wa ukoo

Historia ya Kesi

Agosti 20, 2016, maofisa wa usalama walivamia Jumba la Ufalme la Mayskiy na kupandikiza machapisho yetu ambayo yalikuwa yamepigwa marufuku kuwa “yenye msimamo mkali.” Ingawa akina ndugu walikuwa na video iliyothibitisha kwamba machapisho hayo yalikuwa yamepandikizwa, mahakama ilitoza shirika la kidini la eneo hilo rubo 200,000 (dola 2,634 za Marekani) eti kwa kuvunja sheria. Miezi kadhaa baadaye, kesi ya uhalifu ilifunguliwa dhidi ya Ndugu Zalipayev kwa msingi wa tukio hilo

Mwendesha-mashtaka anadai kwamba Ndugu Zalipayev alisambaza machapisho yaliyopigwa marufuku na kuwatia moyo Mashahidi wengine wa Yehova kutenda matendo ya jeuri dhidi ya washiriki wa dini nyingine. Mashtaka hayo yanategemea sheria inayokataza “kuwatia moyo watu kushiriki utendaji wenye msimamo mkali” (Sehemu ya 1 ya Kifungu 280 cha Sheria ya Uhalifu ya Urusi).

Kesi hiyo imekuwa mahakamani kuanzia Juni 21, 2020. Muda wote wa kesi hiyo, limekuwa jambo la kawaida kwa mashahidi walioletwa na mwendesha-mashtaka kutoa ushahidi unaopingana au unaofunua kwamba mashtaka yao hayana msingi. Kwa mfano, kesi ilipokuwa ikiendelea ilionekana wazi kwamba baadhi ya mashahidi waliodai kumsikia Ndugu Zalipayev akiwachochea wengine watende kwa jeuri hata hawakuwepo kwenye mikutano ambayo jambo hilo linasemekana lilitukia. Isitoshe, baadhi ya mashahidi wa upande wa mwendesha-mashtaka walisema kwamba machapisho yaliyopigwa marufuku yaliyokuwa yamepatikana kwenye Jumba la Ufalme yalipandikizwa na wenye mamlaka.

Ndugu Zalipayev anaposubiri uamuzi wake, tunasali kwamba yeye na familia yake, waendelee kujipatia nguvu na amani kutokana na maneno haya ya Daudi: “Yehova ni nguvu zangu na ngao yangu; moyo wangu unamtumaini yeye. Amenisaidia, na moyo wangu unashangilia.”—Zaburi 28:7.

a Inaweza kubadilishwa