Hamia kwenye habari

Mahakama ya Jiji la Chekhov iliyo katika Eneo la Moscow

MEI 21, 2021
URUSI

Ndugu na Dada Krutyakov, Ndugu Nikiforov, na Ndugu Zherebtsov Wamtegemea Yehova Kesi Yao Inapoendelea Kusikilizwa

Ndugu na Dada Krutyakov, Ndugu Nikiforov, na Ndugu Zherebtsov Wamtegemea Yehova Kesi Yao Inapoendelea Kusikilizwa

HABARI ZA KARIBUNI | Mahakama ya Urusi Yaunga Mkono Uamuzi wa Kuwapa Kifungo cha Nje Ndugu Watatu na Dada Mmoja

Julai 20, 2021, Mahakama ya Eneo la Moscow ilifanya uamuzi wa kudumisha vifungo vya awali vya Ndugu na Dada Krutyakov, Ndugu Nikiforov, na Ndugu Zherebtsov. Hawatahitaji kwenda gerezani wakati huu.

Mei 24, 2021, Mahakama ya Jiji la Chekhov katika Eneo la Moscow iliwahukumu Ndugu na Dada Krutyakov, Ndugu Nikiforov, na Ndugu Zherebtsov. Mahakama hiyo ilimpa Ndugu Krutyakov kifungo cha nje cha miaka sita. Dada Krutyakova, Ndugu Nikiforov, na Ndugu Zherebtsov walihukumiwa kifungo cha nje cha miaka miwili. Hawatahitaji kwenda gerezani wakati huu.

Maelezo Mafupi Kuwahusu

Yuriy Krutyakov

  • Alizaliwa: 1952 (Nizhny Novgorod)

  • Maisha Yake: Anafanya biashara ya uhandisi wa viwandani na ujenzi. Alifanya kazi akiwa msimamizi wa ujenzi na pia ya kuchora ramani. Alitafuta kusudi la Maisha ya binadamu kwa miaka mingi. Mwishowe alipata majibu baada ya kujifunza Biblia na Mashahidi wa Yehova. Alibatizwa mwaka wa 1998

    Alifunga ndoa na Zinaida mwaka wa 2012. Wanapenda kupika na kusikiliza muziki

Zinaida Krutyakova

  • Alizaliwa: 1958 (Nizhnedevitsk)

  • Maisha Yake: Alikuwa akimlea binti yake bila msaada wa mzazi mwingine. Alifanya kazi ya uhandisi wa vyombo vya udongo na bidhaa ambazo zinaweza kuhimili joto kali. Sasa amestaafu

    Alitatizwa sana na ukosefu mwingi wa haki unaoendelea duniani. Alipata majibu yanayoridhisha kwa kujifunza Biblia na Mashahidi wa Yehova. Alibatizwa mwaka wa 2003. Alifunga ndoa na Yuriy mwaka wa 2012

Vitaliy Nikiforov

  • Alizaliwa: 1968 (Nevel, Eneo la Pskov)

  • Maisha Yake: Alipokuwa mtoto, alifaulu sana katika somo la hesabu na alipenda michezo. Alifanya kazi ya kurekebisha ndege katika Jeshi la Angani la Urusi (Russian Air Force)

    Alianza kujifunza Biblia na Mashahidi wa Yehova mwaka wa 2005. Alistaafu jeshini mwaka wa 2007. Alibatizwa mwaka wa 2012

Konstantin Zherebtsov

  • Alizaliwa: 1973 (Turkmenistan)

  • Maisha Yake: Alipokuwa kijana, alifurahia kuinua vyuma na kukusanya stempu za kubandika kwenye barua. Alihitimu katika shule ya ufundi na kufanya kazi akiwa fundi umeme. Tangu 2003, alifanya kazi kwenye kiwanda cha kutegeneza mashine ambazo zingetumiwa katika mfumo wa kutokeza umeme wa nuklia.

    Alifunga ndoa na Natalya mwaka wa 1994. Walijifunza Biblia wakiwa pamoja na Mashahidi wa Yehova. Walibatizwa mwaka wa 2016

Historia ya Kesi

Septemba 30, 2019, Halmashauri ya Uchunguzi ya Urusi iliyo katika eneo la Moscow ilianzisha kesi ya uhalifu dhidi ya Ndugu Vitaliy Nikiforov, Ndugu Konstantin Zherebtsov, Ndugu Yuriy Krutyakov na mke wake, Dada Zinaida Krutyakova. Kisha baada ya siku mbili, wenye mamlaka walifanya msako katika nyumba zao.

Vitaliy, Konstantin, na Zinaida walihojiwa kwa muda mrefu, na baada ya hapo waliwekwa kizuizini kwa usiku mmoja. Kisha wakaachiliwa na kuwekwa katika kifungo cha nyumbani.

Machi 5, 2020, Yuriy alipelekwa mahabusu na tangu wakati huo, amehamishwa na kupelekwa maeneo matatu tofauti. Hadi sasa bado yupo huko.

Konstantin anaeleza kwamba sala imemsaidia kuvumilia jaribu hili. Usiku ambao walifanya msako nyumbani kwake, alimwomba Yehova amsaidie kukabiliana na wasiwasi. Anasema hivi: “Kwa kuwa watulivu na kuwa na mtazamo unaowaonyesha wenye mamlaka kwamba tunawaheshimu, mimi na familia yangu tulitoa ushahidi wa kwamba watu wa Mungu ni wenye amani na wanaotii sheria. Hali inapokuwa ngumu, Andiko la Zekaria 2:8 linanitia moyo na kunipa nguvu. Linanikumbusha kwamba Yehova ananijali na ananithamini; ananihakikishia kwamba atanilinda kama mboni ya jicho lake.”

Kadiri ambavyo ndugu zetu watatu na dada yetu mpendwa wanavyoendelea kumtupia Yehova mizigo yao, tuna uhakika kwamba ataendelea kuwategemeza.—Zaburi 55:22.