Hamia kwenye habari

Maeneo mawili ya Mashahidi wa Yehova yaliyochukuliwa huko St. Petersburg; iliyokuwa ofisi ya tawi huko Solnechnoye (kushoto) na jengo lililokuwa Jumba la Kusanyiko huko Kolomyazhskiy (kulia)

JULAI 4, 2019
URUSI

Serikali ya Urusi Yaendelea Kuchukua Majengo ya Mashahidi wa Yehova Yenye Thamani ya Dola Zaidi ya Milioni 57 za Marekani

Serikali ya Urusi Yaendelea Kuchukua Majengo ya Mashahidi wa Yehova Yenye Thamani ya Dola Zaidi ya Milioni 57 za Marekani

Tangu Aprili 20, 2017, Mahakama Kuu ya Urusi ilipopiga marukufu ibada ya Mashahidi wa Yehova nchini humo, ndugu na dada zetu wameendelea kuteswa na kufungwa gerezani. Serikali imeendelea kuchukua hatua kwa hatua majengo na viwanja 131 vilivyomilikiwa na Mashahidi wa Yehova, na majengo mengine 60 yanakabili hatari ya kuchukuliwa. Inakadiriwa kwamba kwa ujumla viwanja na majengo hayo yana thamani ya dola zaidi ya 57 milioni za Marekani.

Mojawapo ya majengo yaliyochukuliwa ni ofisi ya tawi ya Urusi huko Solnechnoye—ambayo yalikuwa yanamilikiwa na Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania. (Ona picha juu kushoto.) Majengo hayo peke yake yana thamani ya dola milioni 30 hivi za Marekani. Majengo mengeni 43 yaliyochukuliwa yanamilikiwa na mashirika ya kimataifa yaliyo Austria, Denmark, Finland, Uholanzi, Norway, Ureno, Hispania, Sweden, na Marekani. Kuchukuliwa kwa majengo hayo ni kinyume cha sheria, kwa sababu uamuzi wa Mahakama Kuu wa kuwapiga marufuku Mashahidi wa Yehova haukuipa serikali kibali cha kisheria cha kuchukua mali zinazomilikiwa na mashirika ya kimataifa.

Mashahidi wa Yehova wamepeleka mashtaka ya madai kwenye Mahakama ya Ulaya ya Haki za Kibinadamu (ECHR) kuhusu kuchukuliwa isivyo halali kwa iliyokuwa ofisi ya tawi nchini Urusi. Hata mahakama ya ECHR itoe uamuzi gani, tunamtegemea Yehova na tuna uhakika naye. Tunasali kwamba ndugu na dada zetu nchini Urusi waendelee kuwa jasiri wanapoazimia kutoruhusu kuvamiwa, kukamatwa, au kuchukuliwa kwa majengo ya ibada kufanye waache kumwabudu Yehova “kwa roho na kweli.”—Yohana 4:23.