Hamia kwenye habari

Kulingana na jopo la haki za kibinadamu, ndugu na dada hawa kumi, pamoja na wanane wengine, walikamatwa na kuwekwa kizuizini isivyo haki nchini Urusi: Andrey Magliv, Igor Egozaryan, Ruslan Korolev, Vladimir Kulyasov, na Valeriy Rogozin (juu, kuanzia kushoto); Valeriy Shalev, Tatyana Shamsheva, Olga Silayeva, Aleksandr Solovyev, na Denis Timoshin (chini, kuanzia kushoto)

MEI 18, 2020
URUSI

Urusi Ilikiuka Sheria ya Kimataifa kwa Kuwakamata Mashahidi 18 wa Yehova, Lasema Jopo la Wataalamu la Umoja wa Mataifa

Urusi Ilikiuka Sheria ya Kimataifa kwa Kuwakamata Mashahidi 18 wa Yehova, Lasema Jopo la Wataalamu la Umoja wa Mataifa

Jopo la wataalamu kuhusu haki za kibinadamu limetoa hati yenye kurasa 15 inayoonyesha kwamba Urusi ilikiuka sheria ya kimataifa kwa kuwakamata na kuwatia kizuizini Mashahidi 18 wa Yehova katika majiji mbalimbali kuanzia Mei 2018 hadi Julai 2019. Jopo hilo limeagiza Mashahidi ambao bado wako kizuizini waachiliwe mara moja na bila masharti.

Nakala ya awali ya hati ya jopo hilo ilitolewa Mei 15, 2020. Toleo la mwisho litapatikana kwenye tovuti ya Umoja wa Mataifa hivi karibuni.

Hii ndiyo mara ya tatu katika mwaka uliopita kwamba jopo hilo, linaloitwa Kamati ya Umoja wa Mataifa ya Vifungo Visivyo vya Haki, limetoa uamuzi unaowaunga mkono waamini wenzetu. Katika uamuzi wake wa karibuni zaidi, Kamati hiyo ilishutumu mambo mengi yasiyo ya haki yaliyofanywa dhidi ya ndugu na dada zetu.

Ikizungumza kuhusu kutumia “nguvu nyingi kupita kiasi” wakati wa kuwakamata Mashahidi wa Yehova, Kamati hiyo ilisema kwamba “hakuna msingi wa kutetea matendo kama hayo yaliyofanywa na polisi” na ikakazia kwamba “hakuna yeyote kati [ya Mashahidi hao] aliyepaswa kukamatwa na kuwekwa mahabusu na hakuna kesi iliyopaswa kufanywa wala inayopaswa kufanywa dhidi yao.”

Jopo hilo linapinga vikali kwamba Mashahidi hao wamehusika katika utendaji wowote unaodaiwa kuwa wenye msimamo mkali. Linaeleza kwamba ndugu na dada hao hawajafanya lolote isipokuwa kuzingatia “haki yao ya uhuru wa kuabudu kwa amani.”

Katika hati hiyo, wataalamu hao wanapinga mbinu zilizotumiwa mahakama katika kesi dhidi ya ndugu zetu. Kwa mfano, wakati wa kesi moja ya kuongeza muda wa kuwekwa kizuizini, dada wawili walipokuwa mahakamani walifungiwa katika kizimba kama cha kuzuilia wanyama wakali. Kamati hiyo ya Vifungo Visivyo vya Haki inaeleza kwamba sheria ya kimataifa inatambua haki ya watu wote “kuonwa kuwa hawana hatia hadi itakapothibitishwa kupatana na sheria kwamba wana hatia.” Kwa sababu hiyo, dada zetu hawakupaswa kuwa “wamefungwa pingu au kuwekwa katika vizimba vya aina hiyo wakati wa kesi wala hawakupaswa kufikishwa mahakamani katika njia iliyoashiria kwamba huenda wao ni wahalifu hatari.”

Kamati ya Umoja wa Mataifa ya Vifungo Visivyo vya Haki imeagiza kwamba Urusi ifutilie mbali rekodi za uhalifu za Mashahidi wote 18 na kuwalipa ridhaa kupatana na sheria ya kimataifa. Mbali na hilo, nchi hiyo inasihiwa “ihakikishe kwamba uchunguzi kamili na usio wa kiserikali unafanywa ili kufahamu hali zilizoongoza kwenye ukiukaji huo wa haki” na kwamba “ichukue hatua zinazofaa dhidi ya wale waliohusika kukiuka haki za [Mashahidi hao].”

Hati ya kamati hiyo inaonyesha kwamba Mashahidi hao 18 ni “sehemu ya kikundi kinachozidi kuongezeka cha Mashahidi wa Yehova nchini Urusi ambao wamekamatwa, kuzuiliwa, na kuhukumiwa kuwa wahalifu kwa msingi wa kutumia haki yao ya uhuru wa kidini,” haki ambayo inalindwa na mkataba wa kimataifa ulioidhinishwa pia na Urusi. Hivyo, ingawa hati hiyo ya sasa inakazia fikira visa vya ndugu na dada 18 waliotajwa humo, Kamati hiyo ilisema kwamba mambo yaliyotajwa humo “yanawahusu wengine wote walio katika hali kama hizo.”

Ingawa hati hiyo ya Kamati ya Umoja wa Mataifa ya Vifungo Visivyo vya Haki haitoi uhakikisho kwamba ndugu na dada zetu nchini Urusi wataondolewa hatia, kuna tumaini kwamba inaweza kuboresha hali yao. Tunasubiri kuona jibu la Urusi. Kwa sasa, ndugu na dada zetu nchini Urusi wanapoendelea kuvumilia mateso kwa ujasiri, tunajua kwamba Baba yetu mwenye upendo, Yehova, ataendelea kuwapa shangwe na amani kwa sababu ya kumtegemea.—Waroma 15:13.