Hamia kwenye habari

Makao makuu ya Taasisi ya Kitaifa ya Kuchunguza Shughuli za Kifedha

JANUARI 13, 2023
URUSI

Urusi Inaendelea Kuwawekea Mamia ya Mashahidi wa Yehova Vikwazo vya Kiuchumi

Urusi Inaendelea Kuwawekea Mamia ya Mashahidi wa Yehova Vikwazo vya Kiuchumi

Nchini Urusi, Taasisi ya Kitaifa ya Kuchunguza Shughuli za Kifedha (Rosfinmonitoring) ni taasisi ya serikali iliyo na jukumu la kukabiliana na uhalifu wa kiuchumi, kama vile kuzuia mashirika yenye msimamo mkali yasipokee pesa. Taasisi hiyo ina orodha ya watu wanaoshukiwa kuhusika katika utendaji wenye msimamo mkali au wa kigaidi. Mtu anaweza kutiwa kwenye orodha hiyo hata ikiwa mahakama haijathibitisha kuwa ana hatia.

Tangu 2017, Mahakama Kuu ya Shirikisho la Urusi ilipofanya uamuzi wa kupiga marufuku utendaji wa Mashahidi wa Yehova, majina ya ndugu na dada 525 yametiwa katika orodha hiyo. a Idadi hiyo inatia ndani zaidi ya Mashahidi 100 wenye umri mkubwa.

Wote walio kwenye orodha hiyo wamewekewa vikwazo vikali vya kiuchumi. Kwa mfano, hawawezi kupata pesa zilizo kwenye akaunti zao za benki, na wanaruhusiwa tu kutoa angalau rubo 10,000 (dola 137 za Marekani) kwa kila mshiriki wa familia kwa ajili ya matumizi. Pia wamewekewa vizuizi vingine vinavyowazuia au kufanya iwe vigumu sana kushiriki utendaji wa kawaida. Kwa mfano, wanakabili changamoto kubwa wanapotaka kununua au kuuza nyumba au gari, kupata bima, au kupata ridhaa za kutoajiriwa, urithi, au mkopo wa benki. Mashahidi waliostaafu au ambao ni walemavu ndio wanaoathiriwa zaidi kwa sababu wanapambana kulipia matibabu na mara nyingi hawaruhusiwi kutumia usafiri wa umma.

Ndugu Anton Chermnykh anayeishi Ussuriysk, ambaye aliongezwa kwenye orodha hiyo mnamo Desemba 2019 anasema hivi: “Ili kupata mshahara wangu, lazima nithibitishe kila mwezi kwamba nilipata pesa hizo kihalali. Lazima nipeleke stakabadhi nyingi ili wafanyakazi wa benki wazinakili na kuzituma Moscow. Serikali itachukua majuma mawili kuchunguza stakabadhi hizo. Kisha nitarudi kwenye benki hiyo siku niliyoelekezwa ili mfanyakazi wa benki anitolee mshahara kutoka kwenye akaunti yangu, anipe, na kuizuilia akaunti hiyo tena. Wafanyakazi wapya wa benki wanapogundua nipo kwenye orodha ya magaidi, wao huniogopa sana.”

Licha ya changamoto hizo, ndugu na dada zetu wanadumisha mtazamo mzuri. Ndugu Yuriy Belosludtsev, ambaye jina lake lilitiwa katika orodha hiyo kwa miaka miwili na nusu kabla ya kuhukumiwa kifungo cha nje cha miaka sita anasema hivi: “Akaunti zangu zilizuiliwa. Lakini mimi na mke wangu tulisaidiwa na akina ndugu na dada. Tunamshukuru sana Yehova kwa utegemezo wao.”

Tunajua kwamba Yehova anatambua kabisa ukosefu wa haki ambao ndugu na dada zetu nchini Urusi wanakabili. Tunasali tukiwa una uhakika kamili kwamba Yehova ataendelea kuwaandalia mahitaji yao wanapoendelea kukabiliana na jaribu hili.​—Mathayo 6:33.

a Kufikia Desemba 2022, ndugu na dada 35 wameondolewa kwenye orodha ya Rosfinmonitoring baada ya kutumikia kifungo chao au baada ya kulipa faini.