Hamia kwenye habari

Polisi wa eneo na maofisa wa Usalama wa Taifa (FSB) wakivamia nyumba ya ndugu yetu jijini Nizhny Novgorod mwaka 2019

JULAI 15,. 2020
URUSI

Wenye Mamlaka Nchini Urusi Wavamia Idadi Kubwa Zaidi ya Nyumba za Ndugu Zetu

Wenye Mamlaka Nchini Urusi Wavamia Idadi Kubwa Zaidi ya Nyumba za Ndugu Zetu

Kulingana na ripoti rasmi kwa waandishi wa habari, Julai 13, 2020 wenye mamlaka nchini Urusi walivamia nyumba 110 za ndugu zetu katika Eneo la Voronezh wakiwa na bunduki. Hiyo ndiyo idadi kubwa zaidi ya nyumba za ndugu zetu kuvamiwa katika siku moja tangu marufuku ilipoanza mwaka wa 2017. Ndugu wawili, Aleksandr Bokov na Dmitrii Katyrov, walipigwa na kutendewa isivyo haki kwa sababu walikataa kuwapa maofisa hao nywila za simu zao.

Agizo la kufanya uvamizi huo ulitolewa na Mahakama ya Wilaya ya Leninsky iliyoko Voronezh. Maofisa hao walivamia angalau majiji, miji, na vijiji saba katika mkoa huo. Ndugu wengi walikamatwa ili kuhojiwa na Kamati ya Uchunguzi ya eneo hilo.

Julai 14, 2020, siku iliyofuata, Mahakama ya Wilaya ya Leninsky iliagiza ndugu kumi wawekwe kizuizini hadi Septemba 3, 2020: Aleksei Antiukhin mwenye umri wa miaka 44, Sergey Bayev mwenye umri wa miaka 47, Iurii Galka mwenye umri wa miaka 44, Valeriy Gurskiy mwenye umri wa miaka 56, Vitalii Nerush mwenye umri wa miaka 41, Stepan Pankratov mwenye umri wa miaka 24, Igor Popov mwenye umri wa miaka 54, Evgenii Sokolov mwenye umri wa miaka 44, Mikhail Veselov mwenye umri wa miaka 51, Anatoliy Yagupov mwenye umri wa miaka 51.

Ingawa ripoti iliyotajwa hapo juu ilisema ni nyumba 110 zilizovamiwa, tumethibithisha habari hiyo kwa kuwasiliana na familia 100 za Mashahidi ambao nyumba zao na mali zao zilipekuliwa. Idadi hiyo inaweza kuongezeka. Ni changamoto kuwasiliana na ndugu wote ambao nyumba zao zilivamiwa kwa sababu simu na kompyuta zao zilichukuliwa wakati wa tukio hilo.

Hapo awali, idadi kubwa zaidi ya nyumba kuvamiwa kwa siku moja ilifanyika Februari 10, 2020 kwa kuwa wenye mamlaka walivamia nyumba 50 za Mashahidi katika Eneo la Transbaikal. Tangu uamuzi wa Mahakama Kuu utolewe mwaka 2017, zaidi ya nyumba 1,000 za ndugu zetu zimevamiwa.

Kwa kuwa tunaelewa unabii wa Biblia, hatushangazwi na majaribu haya ambayo ndugu zetu nchini Urusi na wale walio katika nchi nyingine wanakabiliana nayo. Tunaendelea kusali kwa ajili ya ndugu zetu, tukiwa na uhakika kwamba Yehova atawapa roho takatifu kulingana na uhitaji wao ili waendelee kuwa waaminifu.—1 Petro 4:12-14, 19.