Hamia kwenye habari

Hofburg Palace huko Vienna, Austria, ambapo Machi 12, 2020 Baraza la Kudumu la Shirika la Usalama na Ushirikiano wa Ulaya (OSCE) lilizungumzia mateso ya Mashahidi wa Yehova

MEI 1, 2020
URUSI

Wenye Mamlaka wa Ulaya Washutumu Mateso ya Mashahidi wa Yehova Nchini Urusi

Wenye Mamlaka wa Ulaya Washutumu Mateso ya Mashahidi wa Yehova Nchini Urusi

Machi 12, 2020, nchi zaidi ya 30 za Ulaya zilishutumu vikali mnyanyaso na mateso dhidi ya ndugu zetu nchini Urusi. Shutuma hiyo ya kimataifa ilitokea kwenye mkutano ulioandaliwa na Baraza la Kudumu la Shirika la Usalama na Ushirikiano wa Ulaya (OSCE). Mojawapo ya malengo ya OSCE ni kulinda haki za kibinadamu.

Katika maelezo ya pamoja yaliyotolewa mbele ya Baraza la Kudumu la OSCE, mataifa 27 ya Muungano wa Ulaya, pamoja na mataifa mengine 6 ambayo si washirika wa muungano huo, yalisema hivi: “Muungano wa Ulaya unaendelea kusikitishwa na hali ya Mashahidi wa Yehova nchini Urusi ambao wanateswa kimakusudi, kwa kuvamiwa nyumbani, kuwekwa mahabusu bila sababu, kufanyiwa uchunguzi wa kihalifu, na hata kufungwa kwa miaka saba. Isitoshe, tunahangaishwa sana na ripoti za karibuni za kwamba walinzi wa magereza na polisi wamewatesa na kuwatendea vibaya baadhi ya Mashahidi wa Yehova walio kizuizini au kabla ya kuwapeleka kizuizini.”

Balozi wa Uingereza katika OSCE, Neil Bush, alisema hivi katika hotuba yake mbele ya Baraza hilo la Kudumu: “Uamuzi wa Julai 2017 wa Mahakama Kuu ya Urusi, uliopinga rufaa dhidi ya uamuzi uliowatambulisha Mashahidi wa Yehova kuwa ‘watu wenye msimamo mkali,’ ulifanya ibada yenye amani ya raia 175,000 wa Urusi kuwa ya uhalifu na kukiuka haki ya uhuru wa kidini iliyo katika Katiba ya Urusi na katika vifungu vingi vya katiba ya OSCE.” Aliendelea kusema hivi: “Tangu uamuzi huo ulipotolewa, tumeona ongezeko katika idadi ya vifungo, uchunguzi wa kihalifu, na kesi dhidi ya Mashahidi wa Yehova kote nchini Urusi. Kama shirika la OSCE, tungependa kurudia kutaja hangaiko letu dhidi ya mateso na kutendewa vibaya kwa Mashahidi wa Yehova.”

Moja kati ya visa vinavyotajwa na wenye mamlaka wa Ulaya ni kile cha Februari 6, 2020, ambapo Mashahidi watano walipigwa. Walinzi wa gereza katika Gereza Na. 1 la Urusi waliwapiga Ndugu Aleksey Budenchuk, Gennadiy German, Roman Gridasov, Feliks Makhammadiyev, na Aleksey Miretskiy. Jopo la Muungano wa Ulaya liliripoti hivi: “Wote watano wana majeraha mabaya na mmoja wao [Feliks Makhammadiyev] anahitaji kulazwa hospitalini. Mbali na hilo, Februari 10, 2020, iliripotiwa kwamba Vadim Kutsenko aliteswa kabla ya kupelekwa kizuizini. Polisi walimpiga tena na tena na kumnyonga na kupiga kwa umeme, huku wakidai awape habari kuhusu Mashahidi wengine wa Yehova.”

Jopo hilo la Muungano wa Ulaya lilisema kwamba “mateso na kutendewa vibaya kwa njia nyingine ni ukiukaji mkubwa sana wa haki na heshima za kibinadamu. Mateso huvunja sheria za kimataifa za haki ya kibinadamu, hasa Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kiraia na Kisiasa, Mkataba wa Ulaya wa Haki za Kibinadamu, na Kongamano la Umoja wa Mataifa dhidi ya Mateso na Matendo au Adhabu Nyingine ya Kikatili, ya Kinyama, na Yenye Kushushia Hadhi, ambazo Shirikisho la Urusi lilikubali kutii.”

Isitoshe, viongozi hao wa Ulaya walitambua kwamba matendo dhidi ya Mashahidi wa Yehova nchini Urusi yanapinga moja kwa moja ahadi ambazo Shirikisho la Urusi lilitoa mbele ya Baraza la Kudumu kuonyesha kwamba ndugu na dada zetu walikuwa huru kuendeleza ibada yao nchini humo.

Jopo hilo la Muungano wa Ulaya lilisema hivi: “Aprili 20, 2017, Mahakama Kuu ya Shirikisho la Urusi ilipiga marufuku Kituo cha Usimamizi cha Mashahidi wa Yehova na mashirika yote nchini humo kwa msingi wa ‘utendaji wenye msimamo mkali.’ Baada ya hapo, tumesikia Jopo la Urusi likidai zaidi ya mara moja mbele ya Baraza la Kudumu kwamba Mashahidi wa Yehova wako, na wataendelea, kuruhusiwa kuendeleza ibada au imani yao kwa uhuru kamili. Hata hivyo, tunaendelea kusikia kwamba Mashahidi wa Yehova wanavamiwa nyumbani, wanafungwa bila sababu, na kufanyiwa uchunguzi wa kihalifu.”

Viongozi wa Muungano wa Ulaya walisema kwamba “tangu marufuku dhidi ya mashirika yote ya kidini ya Mashahidi wa Yehova nchini Urusi, nyumba 869 zimefanyiwa msako, watu 26 wako mahabusu, 23 wako katika kifungo cha nyumbani, 316 wamefunguliwa mashtaka, na 29 wamefungwa.”

Balozi Bush alisema hivi: “Ni wazi kutokana na idadi zilizotajwa kwamba Mashahidi wa Yehova wanapojihusisha na shughuli zozote za kidini, nyumba zao zinaweza kufanyiwa msako, wanaweza kuwekwa kizuizini kwa muda mrefu, kushtakiwa kwa uhalifu, na kufungwa. Idadi ya nyumba zinazovamiwa, kutia ndani uvamizi unaofanywa ndani ya siku moja katika jiji moja, unatokeza wazo kwamba kuna kampeni iliyopangwa ya kuwatesa Mashahidi wa Yehova.”

Wataalamu wa uhuru wa kidini wameshutumu pia mateso hayo dhidi ya ndugu zetu nchini Urusi. Akizungumza kuhusu maelezo ya Jopo la Muungano wa Ulaya, Dakt. Gudrun Kugler, wakili, mwanasiasa, na mwanatheolojia wa Kanisa Katoliki kutoka Austria, alisema hivi: “Hali zimezorota ghafla tangu Mashahidi wa Yehova walipopigwa marufuku Aprili 2017. . . . Vifungo vyote vya Mashahidi wa Yehova nchini Urusi vinategemea sheria dhidi ya msimamo mkali wa kidini ambayo imeshutumiwa na mashirika ya haki za kibinadamu kuwa ‘haieleweki na ni pana kupita kiasi.’ Kutambuliwa tu kuwa Shahidi wa Yehova na kuendeleza shughuli za kidini kunaweza kumfanya mtu afugwe gerezani kwa kutegemea Kifungu Na. 282.2. . . . Mateso makali dhidi ya Mashahidi wa Yehova na dini nyingine ndogo nchini Urusi yanapaswa kukomeshwa!”

Muungano wa Ulaya ulisema kwamba Urusi na nchi wanachama wa OSCE “zina wajibu wa kuchukua hatua madhubuti kuzuia mateso, kuwahukumu waliowatesa wengine, kuwatafuta walioathiriwa, na kuhakikisha walioathiriwa wamelipwa fidia. Kwa hiyo, tunaliomba Shirikisho la Urusi lifanye uchunguzi wa haraka na wenye kina kuhusu ripoti zote za matendo hayo, ili kuhakikisha kwamba wahusika wameadhibiwa. . . . Tunawaomba wenye mamlaka wafute mashtaka yote dhidi ya watu ambao wameshtakiwa au kufungwa isivyo haki kwa kutenda kupatana na haki zao za kibinadamu. Tunaliomba Shirikisho la Urusi litende kupatana na ahadi iliyotoa mbele ya nchi nyingine zote ya kulinda haki za kibinadamu, uhuru wa kusema, kushirikiana, kukusanyika kwa amani, dini au imani kutia ndani haki za mtu za kuwa katika kikundi kidogo, na haki ya kesi kusikilizwa kupatana na sheria.”

Iwe Urusi itatenda kupatana na shutuma hizo za kimataifa na kuheshimu uhuru wa ibada au la, tunajua kwamba Yehova ataendelea kuwasaidia ndugu na dada nchini Urusi kuvumilia kwa subira na ujasiri hadi haki ya kweli itakaposhinda.—Zaburi 10:18.