SEPTEMBA 25, 2020
URUSI
Wenzi wa Ndoa wa Kwanza Kuwekwa Mahabusu Nchini Urusi Wakabili Kifungo Wakiwa na Dada Wawili
Hukumu Inatarajiwa
Oktoba 21, 2020, a Mahakama ya Wilaya ya Pervomayskiy katika Jiji la Omsk itatangaza uamuzi wake katika kesi dhidi ya Ndugu Sergey Polyakov na mke wake, Anastasia, pamoja na Dada Gaukhar Bektemirova na Dada Dinara Dyusekeyeva. Mwendesha-mashtaka aliiomba mahakama imfunge Ndugu Polyakov miaka sita na nusu gerezani. Dada hao watatu wanakabili kifungo cha nje cha miaka miwili.
Maelezo Mafupi Kuwahusu
Sergey Polyakov
Tarehe ya Kuzaliwa: 1972 (Eneo la Murmansk)
Maisha Yake: Anafanya kazi akiwa mwanafizikia na alifunga ndoa na Anastasia mwaka wa 2003
Anastasia Polyakova
Tarehe ya Kuzaliwa: 1984 (Eneo la Murmansk)
Maisha Yake: Amesomea sheria. Yeye na Sergey wanafurahia kujifunza lugha kama vile Kichina, Kikazakh, Lugha ya Ishara ya Urusi, na Kiserbia
Gaukhar Bektemirova
Tarehe ya Kuzaliwa: 1976 (Uryl, Kazakhstan)
Maisha Yake: Mtoto wa mwisho kati ya watoto sita. Amelelewa katika eneo la milima ya Kazakhstan na anapenda mazingira ya asili. Alitumia miaka mingi akijiuliza kusudi la maisha ni nini. Hatimaye, akapata majibu yanayopatana na akili na yanayoridhisha katika Biblia. Kujifunza kwa kina Neno la Mungu kumemwimarisha na kumfariji licha ya kuwa kizuizini
Dinara Dyusekeyeva
Tarehe ya Kuzaliwa: 1982 (Leningradskoye, Kazakhstan)
Maisha Yake: Alipokuwa msichana alitafakari sana kuhusu kusudi la maisha. Akaanza kujifunza Biblia alipokuwa na umri wa miaka 17. Alithamini hekima aliyojifunza katika Biblia na alisisimka sana alipolijua jina la Mtungaji wake, yaani Yehova. Anafurahia kucheza mpira wa kikapu, mpira wa wavu, kukimbia, na kuendesha baiskeli
Historia ya Kesi
Usiku wa Julai 4, 2018, Ndugu Polyakov na mke wake, Anastasia, walikuwa wamelala, kikundi cha polisi walipovunja mlango na kuingia ndani ya nyumba yao. Maofisa waliokuwa wamejifunika uso walimpiga vibaya sana Ndugu Polyakov. Maofisa hao waliwakamata wenzi hao na kuwapeleka mahabusu. Wakawa wenzi wa ndoa wa kwanza kufungwa baada ya uamuzi wa Mahakama Kuu wa mwaka wa 2017 uliopiga marufuku utendaji wa Mashahidi wa Yehova. Familia ya Polyakov ilitenganishwa kwa miezi mitano kwa kuwa kila mmoja wao alifungwa kifungo cha upweke. Baada ya hilo, waliwekwa chini ya ulinzi kwa miezi mitatu katika nyumba yao.
Mei 2019, wenye mamlaka walianza tena kuvamia nyumba za Mashahidi wa Yehova katika Eneo la Omsk kinyume na sheria. Na kwa sababu hiyo Dada Bektemirova na Dada Dyusekeyeva walikamatwa. Kesi zao zimeambatanishwa pamoja na kesi ya uhalifu dhidi ya familia ya Polyakov. Kesi hiyo ilianza Aprili 1, 2020.
Tuna uhakika kwamba Yehova atawaimarisha watumishi wake ili waweze kuvumilia ukosefu huo wa haki.—Waefeso 3:20.
a Inaweza kubadilishwa