Hamia kwenye habari

MEI 31, 2018
URUSI

Shahidi Mwingine wa Yehova Nchini Urusi Ashtakiwa kwa Madai ya Kuwa na Msimamo Mkali

Shahidi Mwingine wa Yehova Nchini Urusi Ashtakiwa kwa Madai ya Kuwa na Msimamo Mkali

Arkadya Akopyan, Shahidi wa Yehova mwenye umri wa miaka 70 ambaye amestaafu kazi ya kushona nguo, ameshtakiwa yapata mwaka mmoja sasa kwa madai ya kushiriki utendaji wenye msimamo mkali. Ikiwa atapatikana na hatia, atatozwa faini kubwa au kifungo cha kufikia miaka minne gerezani.

Mwendesha-mashtaka anadai kwamba Bw. Akopyan ana hatia ya “kuchochea chuki ya kidini” kwa kutegemea hotuba ya kidini aliyotoa kwenye Jumba la Ufalme mahali ambapo amekuwa akihudhuria kwa miaka mingi. Katika mahakama, mwendesha-mashtaka alitegemea sana ushahidi wa uwongo wa watu sita ambao si Mashahidi wa Yehova. Walidai kwamba Bw. Akopyan alitoa kauli za kashfa wakati wa hotuba yake na aliwapa machapisho yanayochochea “msimamo mkali” ili wakawape watu wengine.

Bw. Akopyan na wengine ambao wanamjua vizuri walikataa madai hayo. Wakili wake alipeleka uthibitisho mahakamani kwamba watu hao sita waliotoa madai hayo hawaishi karibu na jengo ambalo Bw. Akopyan inadaiwa alitoa maelezo hayo. Isitoshe, Mashahidi wa Yehova hawana mpango wa kuwapa machapisho ya kidini watu ambao si Mashahidi ili wakawagawie wengine. Mke wa Bw. Akopyan, Sonya, ambaye si Shahidi wa Yehova, aliieleza mahakama wakati akihojiwa kwamba amekuwa katika ndoa yenye furaha kwa miaka 40 na kwamba mume wake hajawahi kamwe kumlazimisha ndugu yake yeyote wa ukoo awe Shahidi wa Yehova.

Hakimu Oleg Golovashko aliamuru uchunguzi wa kitaalamu ufanywe kuchunguza maelezo yaliyotolewa na Bw. Akopyan wakati akitoa hotuba yake ili kuthibitisha ikiwa alikuwa ‘akichochea chuki ya kidini.’ Kesi hiyo ya Bw. Akopyan iliposikilizwa Mei 15, 2018, hakimu alieleza kwamba uchunguzi wa kitaalamu unapaswa ukamilike mwezi Septemba 2018 lakini kesi itakuwa ikiendelea. Kesi hiyo imeratibiwa isikilizwe tena Juni 5, siku hiyo Bw. Akopyan atahojiwa. Ingawa hajawekwa mahabusu, Bw. Akopyan amewekewa vizuizi vya kusafiri tangu kesi yake ilipoanza kusikilizwa mnamo Mei 2017 katika Mahakama ya Wilaya ya Prokhladny.

Gregory Allen, Wakili Mshiriki wa Mashahidi wa Yehova, alisema hivi: “Bw. Akopyan ni mmoja kati ya waathiriwa wa matumizi mabaya ya sheria ya Urusi ya msimamo mkali inayotekelezwa dhidi ya Mashahidi wa Yehova. Yeye ni mtu mnyoofu, raia anayetii sheria ambaye anataka kumwabudu Mungu kwa amani. Uvamizi wa serikali dhidi ya Mashahidi wa Yehova unaotokana na taarifa za uwongo umefanya kila Shahidi akabili vitisho na umeondoa kiungo muhimu cha muungano wa jamii katika nchi.”

Bw. Akopyan ni Shahidi wa pili nchini Urusi ambaye ameshtakiwa isivyo haki kwa sababu ya “msimamo mkali.” Kesi ya uhalifu ya Dennis Christensen, Shahidi jijini Oryol, ilianza Februari 2018. Amekuwa mahabusu kwa mwaka mmoja na anaweza kukabili kifungo cha hadi miaka kumi gerezani akipatikana na hatia. a Mashahidi wengine saba wapo mahabusu katika maeneo mbalimbali ya Urusi lakini hawajashtakiwa rasmi.

a Wanaume wote wawili wameshtakiwa kulingana na Sheria ya Uhalifu lakini kwenye vifungu tofauti. Bw. Akopyan alishtakiwa kulingana na kifungu cha 282(1) cha Sheria kwa madai ya kuchochea chuki ya kidini. Dennis Christensen alishtakiwa kwa kukiuka kifungu cha 282.2(1) cha Sheria ya Uhalifu kwa madai ya kupanga utendaji wa shirika la kidini ambalo lina msimamo mkali. Mtu hupewa adhabu kubwa zaidi akikiuka sheria hii.