NOVEMBA 29, 2018
URUSI
Dennis Christensen Aungwa Mkono na Jamii ya Kimataifa
Ndugu Dennis Christensen amekuwa gerezani kwa siku zaidi ya 525. Alikamatwa kwa kushiriki utendaji wa imani yake na amesimamishwa mahakamani mara 50 hivi. Mahakama ya Wilaya ya Zheleznodorozhniy iliyoko Oryol, Urusi, inachunguza kesi ya Dennis ambayo inatarajiwa kusikilizwa hadi katikati ya mwezi wa Desemba. Ingawa amefungwa kwa zaidi ya miezi 18, Dennis bado ana mtazamo mzuri na hajapoteza shangwe yake. Bila shaka huo ni uthibitisho kwamba Yehova anamtegemeza kwa kujibu sala za mamilioni ya ndugu zetu ulimwenguni pote.
Dennis amepokea kadi na michoro mingi kutoka kwa Mashahidi wenzake nchini Urusi na kutoka nchi nyingine wakimweleza kwamba wanamuunga mkono kwa upendo. Ndugu walipokuja kusikiliza kesi yake Oktoba 30, Dennis aliwaonyesha kupitia kioo baadhi ya kadi na picha ambazo watoto wamemtumia, wote walifurahia kuziona.
Zaidi ya ndugu zetu ulimwenguni pote, jamii ya kimataifa imependezwa sana na kesi ya Dennis. Julai 21, 2017, Kituo cha Moscow cha Haki za Kibinadamu kilisema kwamba Dennis ni mfungwa wa kisiasa. Juni 20, 2018, Baraza la Urusi la Haki za Kibinadamu liliomba Ofisi ya Mwendesha-Mashtaka ithibitishe uhalali wa kuwafunga Mashahidi wa Yehova kama wahalifu. Septemba 26, 2018, Tume ya Uhuru wa Ibada wa Kimataifa ya Marekani imemworodhesha Dennis kuwa “mfungwa wa kidini kwa sababu ya dhamiri.”
Wakati wa kusikilizwa kwa kesi, Urusi ilisema kwamba marufuku dhidi ya mashirika ya kisheria ya Mashahidi wa Yehova haingeathiri haki za ibada za Shahidi mmoja-mmoja . Maofisa wa kutekeleza sheria wamepuuza hayo na kutumia vibaya sheria ili kutetea uamuzi wao wa kumkamata Dennis na wengine wengi, na kuwashtaki kwa kushiriki utendaji wenye “msimamo mkali.” Mwaka huu, nchi ya Urusi imevamia maeneo kadhaa nchini humo. Kufikia wakati ripoti hii inachapishwa, ndugu na dada 25 wako gerezani, 18 wanatumikia kifungo cha nyumbani, na zaidi ya 40 wamewekewa vizuizi mbalimbali. Matokeo ya kesi ya uhalifu ya Dennis huenda ikaathiri Mashahidi wengine zaidi ya 90, katika maeneo 30 hivi ya Urusi, ambao wanasubiri hukumu itolewe kuhusu kesi zao za uhalifu.
Tunajua kwamba familia yetu ya kimataifa itaendelea kusali kwamba Yehova aendelee kuwaimarisha na kuwatia moyo ndugu na dada zetu wapendwa wanaokabili mashtaka ya uhalifu kwa sababu ya imani, huku tukitazamia kwa hamu siku ambayo ‘atawatendea haki.’—Luka 18:7.