Maelezo Mafupi Kuhusu Urusi
Mwanzoni Mashahidi wa Yehova walifurahia uhuru wa ibada baada ya Shirikisho la Urusi kuwapa usajili wa kitaifa mwaka 1992. Mashahidi walisajiliwa tena mwaka 1999 chini ya Sheria Inayohusu Uhuru wa Dhamiri na Mashirika ya Dini. Kuna mashirika mengi ya kidini ya Mashahidi wa Yehova yaliyosajiliwa na kufanya kazi kotekote nchini humo.
Hata hivyo, Mashahidi wa Yehova wanakabili hali ngumu ambayo inaathiri uhuru wao wa ibada. Tangu mwaka 2009, vyombo vya kulinda usalama vimeunga mkono kampeni ya nchi nzima dhidi ya Mashahidi kwa kuitumia vibaya Sheria ya Kupambana na Shughuli Zenye Msimamo Mkali. Mahakama za Urusi zimetangaza machapisho mengi ya Mashahidi wa Yehova kuwa yana msimamo mkali wa dini, kutia ndani tovuti ya Mashahidi ya jw.org. Polisi wamepekua nyumba nyingi na majengo ya ibada ya Mashahidi. Waendesha mashtaka wamewashtaki Mashahidi kwa makosa ya kupinga serikali na makosa ya jinai kwa sababu tu ya kuhudhuria au kuendesha mikutano ya dini.
Licha ya Mahakama ya Ulaya ya Haki za Binadamu na Mashirika mengine ya kimataifa kupinga mambo hayo, wenye mamlaka nchini Urusi hawafanyi jitihada yoyote kuondoa ubaguzi na usumbufu wanaopata Mashahidi wa Yehova. Vyombo vinavyolinda usalama vimeendelea kuongeza jitihada zao hatua kwa hatua ili kuzuia utendaji wa Mashahidi wa Yehova.