Hamia kwenye habari

JANUARI 21, 2014
URUSI

Maofisa wa Urusi Wataka Mahakama Ipige Marufuku Tovuti Maarufu ya Elimu ya Biblia

Maofisa wa Urusi Wataka Mahakama Ipige Marufuku Tovuti Maarufu ya Elimu ya Biblia

ST. PETERSBURG, Urusi—Agosti 7, 2013, Mahakama ya Wilaya ya Tsentralniy katika jiji la Tver, lililoko kilomita 160 hivi kaskazini ya Moscow, iliamua kwamba tovuti ya jw.org inayotoa elimu ya Biblia inapaswa kupigwa marufuku katika Shirikisho la Urusi.

Ingawa tovuti ya jw.org inatumiwa na mamia ya maelfu ya watu ulimwenguni pote na inaheshimiwa sana na watu wanaofanya utafiti, mahakama hiyo iliunga mkono maofisa waliokuwa wakitaka kupiga marufuku tovuti hiyo. Mahakama hiyo ilitoa uamuzi bila kuijulisha Watchtower Bible and Tract Society of New York, ambao ndio wachapishaji wa tovuti hiyo, wala haikusikiliza upande wao. Mashahidi wa Yehova wanakata rufani kupinga uamuzi huo uliotolewa na Mahakama ya Mkoa wa Tver. Kesi hiyo imepangwa kusikilizwa Januari 22, 2014.

Rufani hiyo ikikataliwa, tovuti hiyo haitapatikana tena kwa ajili ya Mashahidi wa Yehova zaidi ya 160,000 wanaoitumia kwa ajili ya mambo ya kidini na kwa ajili ya funzo la kibinafsi na la familia. Litakuwa tendo la uhalifu kuwatangazia watu kuhusu tovuti hiyo nchini Urusi. Zaidi ya hilo, watu milioni 142 wanaoishi nchini Urusi watazuiwa wasipate habari za Biblia zilizomo katika tovuti ya jw.org ambazo hutolewa bila malipo. Akizungumza kuhusu jambo hilo, Yekaterina Elbakyan, Daktari wa Falsafa na mtaalamu wa mafunzo ya kidini anayetumika akiwa profesa katika Chuo cha Mahusiano ya Kazi na ya Jamii jijini Moscow, anasema kwamba tovuti ya jw.org ni “zawadi kwa ajili ya mtu yeyote anayefanya utafiti kuhusu mambo ya kidini. Ina habari nyingi sana zinazoeleweka kwa urahisi. Mambo muhimu ya kiroho na ya maadili yanazungumziwa kwa njia rahisi sana. Unapotumia tovuti hiyo, unahisi kana kwamba unakaribishwa kwa mikono miwili ndani ya nyumba ya Mashahidi wa Yehova.”

Akizungumza kutoka St. Petersburg, Grigory Martynov, msemaji wa Mashahidi wa Yehova nchini Urusi, alisema hivi: “Tovuti ya jw.org ni kifaa cha pekee kwa ajili ya watu katika nchi yetu wanaotafuta habari kuhusu Biblia na haina uhusiano wowote na mambo ya kisiasa wala ya kibiashara. Tunatumaini kwamba Mahakama ya Mkoa wa Tver itahakikisha kwamba kifaa hiki chenye thamani kinachotoa elimu kitaendelea kupatikana kwa ajili ya watu wote nchini Urusi.”

J. R. Brown, msemaji wa Mashahidi wa Yehova katika makao makuu ya ulimwenguni pote ya Mashahidi wa Yehova jijini New York, alisema hivi: “Tovuti ya jw.org inathaminiwa sana kwa sababu ni kifaa cha kufanyia utafiti na pia inatoa habari zenye kuaminika kwa ajili ya familia ulimwenguni pote. Inathaminiwa sana hivi kwamba kwa wastani watu 900,000 hutembelea tovuti hiyo kila siku ili kupata habari muhimu katika lugha 600 hivi. Haipatani na akili hata kidogo kupiga marufuku habari hizo.”

Wanahabari wanaweza kuwasiliana na:

J. R. Brown, Ofisi ya Habari za Umma, simu +1 718 560 5000

Urusi: Grigory Martynov, simu +7 812 702 2691