Hamia kwenye habari

Maeneo yaliyovamiwa nchini Urusi

MEI 2, 2018
URUSI

Kampeni ya Kuwatisha Mashahidi wa Yehova Yaanza Nchini Urusi

Kampeni ya Kuwatisha Mashahidi wa Yehova Yaanza Nchini Urusi

Polisi katika majiji sita hivi nchini Urusi wamefanya uvamizi mkubwa kwa Mashahidi wa Yehova. Katika kile kinachoonekana kuwa kampeni iliyopangwa, polisi wa kikosi maalumu, wakiwa wameziba nyuso zao na wamebeba bunduki, wamevamia nyumba za Mashahidi, wamewatisha kwa kuwanyooshea bunduki, na kuwakamata vijana kwa wazee ili kuwahoji.

Arkadya Akopyan, na mke wake, Sonya, na wajukuu wao wawili

Mwaka uliopita tu, wenye mamlaka walianza kufanya uchunguzi wa makosa kumi ya uhalifu na kuwafunga gerezani Mashahidi watano kutia ndani Dennis Christensen, ambaye amekuwa mahabusu tangu Mei 25, 2017. Shahidi mwingine mwenye umri wa miaka 69 anayeitwa Arkadya Akopyan, kwa sasa ameshtakiwa katika Jamhuri ya Kabardino-Balkaria. Wote hao wanaweza kukabili kifungo cha miaka miwili hadi kumi kwa sababu tu ya kukutanika pamoja kwa ajili ya ibada.

Aprili 20, 2017, Mahakama Kuu ya Shirikisho la Urusi ilipiga marufuku Kituo cha Usimamizi cha Mashahidi wa Yehova na kuyafunga Mashirika yote 395 ya kisheria ya Mashahidi. Wakati wa kesi kwenye Mahakama Kuu, serikali ya Urusi ilisema kwamba ingawa wameyafunga mashirika yote ya kisheria ya Mashahidi wa Yehova, watu mmoja-mmoja wanaweza kuwa huru kuendelea na imani yao. Hata hivyo, serikali haitendi kupatana na maneno hayo.

Wenye mamlaka nchini Urusi wamefanikiwa kufunga mashirika ya kisheria ya Mashahidi wa Yehova na wameanza kutaifisha majengo yao, sasa wameanza kuwashambulia Mashahidi wenyewe na ibada yao. Kwa sasa ni kosa la jinai kwa Mashahidi wa Yehova zaidi ya 175,000 nchini Urusi kushiriki katika ibada yao.

Kuvamiwa, Kuhojiwa, Kuwekwa Mahabusu

Tangu Januari 2018, maofisa wa polisi wameongeza kasi ya kuwalenga Mashahidi wa Yehova.

Aprili 20, 2018, Shuya, Eneo la Ivanovo: Maofisa wa polisi walipekua nyumba za Mashahidi wanne. Maofisa hao walimchukua Dmitriy Mikhailov na kumpeleka kwenye kituo cha polisi, wakamweka mahabusu, na baadaye wakamwachilia. Wenye mamlaka walianzisha uchunguzi wa kosa la uhalifu na kumshtaki kulingana na Sheria ya Uhalifu ya 282.2(2) kwa ‘kushiriki katika utendaji wa shirika lenye msimamo mkali.’ Amekatazwa kusafiri nje ya mji wa Shuya hadi atakapopewa taarifa.

Aprili 19, 2018, Vladivostok: Polisi na Maofisa wa Usalama wa Taifa (FSB) walivamia nyumba na kumchukua Valentin Osadchuk na wanawake wazee watatu kuwapeleka kituo cha polisi kwa ajili ya kuwahoji. Wenye mamlaka walimshtaki Bw. Osadchuk kulingana na Sheria ya Uhalifu ya 282.2(2), ambapo kupitia sheria hiyo, mtu anaweza kuhukumiwa kifungo cha miaka mawili hadi minne, na wakamweka mahabusu. Aprili 23, Mahakama ya Wilaya ya Frunzenskiy iliamuru kwamba Bw. Osadchuk aendelee kuwa mahabusu hadi Juni 20, 2018. Kwa sasa, yuko mahabusu kwenye gereza la uchunguzi Na. 1 jijini Vladivostok.

Aprili 18, 2018, Polyarny, Eneo la Murmansk: Jioni siku hiyo, polisi wa kawaida na maofisa wa polisi wa kikosi maalumu walioziba nyuso, wakiwa na bunduki walivunja mlango wa nyumba ya familia ya Roman Markin. Maofisa hao walimlazimisha alale chini huku wakimwelekezea bunduki. Binti yake ambaye ni tineja, alipoona kile wanachofanya maofisa wa polisi, alianguka chini na kuficha kichwa chake kwa mikono yake. Polisi walipekua nyumba yote, na baada ya upekuzi walimpeleka Bw. Markin kwenye kituo cha polisi na kumweka mahabusu.

Siku hiyo jioni, polisi walipekua pia nyumba 14 za Mashahidi wengine katika eneo hilo na walipora simu zao, kompyuta zao ndogo, na vitu vingine vya kibinafsi. Kisha, polisi hao waliwapeleka kwenye kituo cha polisi kwa ajili ya kuwahoji. Wenye mamlaka waliwafungulia Bw. Markin na Viktor Trofimov, Shahidi wa Yehova anayeishi katika eneo hilo, kesi ya uhalifu. Wote wawili walishtakiwa kulingana na Sheria ya Uhalifu ya 282.2(1) kwa ‘kupanga utendaji wa shirika lenye msimamo mkali.’ Ikiwa watapatikana na hatia, wanaweza kukabili kifungo cha miaka sita hadi kumi gerezani. Wote wawili wamewekwa mahabusu katika gereza Na. 1 jijini Murmansk.

Aprili 10, 2018, Wilaya ya Zaton, Ufa: Kati ya saa 12:30 asubuhi hadi saa 1:00 asubuhi, wachunguzi na maofisa wa kikosi maalumu cha polisi walivamia na kupekua nyumba kadhaa za Mashahidi. Wakati wakifanya upekuzi huo, maofisa hao waliwahoji Mashahidi. Katika kisa kimoja, ofisa alimwambia mtu mmoja hivi: “Tutakuachia sasa hivi ikiwa utakiri kwamba wewe si mshiriki wa shirika la Mashahidi wa Yehova.” Katika kisa kingine, ofisa alimwambia hivi Shahidi: “Tutawaondoa duniani.” Mashahidi hao wote walipelekwa kwenye kituo cha polisi kwa ajili ya kuchukuliwa alama za vidole na kuhojiwa zaidi.

Walipovamia nyumba ya Bw. na Bi. Khafizov, maofisa waliwanyooshea silaha zao na kuanza kupekua nyumba yao. Baada ya kupekua, polisi walimshika Bi. Khafizova na kumsukumia kwenye gari la polisi, nao wakampeleka kwenye kituo cha polisi kwa ajili ya mahojiano. Bw. Khafizov si Shahidi wa Yehova.

Anatoliy na Alyona Vilitkevich, kabla hajakamatwa

Maofisa walivamia nyumba ya Anatoliy Vilitkevich na kumkamata. Walimwambia mke wake kwamba hatamwona mume wake kwa “muda mrefu sana.” Wenye mamlaka walimshtaki kulingana na Sheria ya Uhalifu ya 282.2(1) kwa ‘kupanga utendaji wa shirika lenye msimamo mkali’ na wamemweka mahabusu hadi Juni 2, 2018. Ikiwa atapatikana na hatia, anaweza kukabili kifungo cha hadi miaka kumi gerezani.

Machi 2018, Oryol: Zaidi ya kesi ya uhalifu ya Dennis Christensen inayoendelea, wenye mamlaka walianza kumchunguza Shahidi mwingine, anayeitwa Sergey Skrynnikov, na Mei 2017 walipekua nyumba saba jijini Oryol. Bw. Skrynnikov bado hajaandikiwa shtaka rasmi. Lakini inadaiwa anashtakiwa kulingana na Sheria ya 282.2(2) kwa ‘kushiriki katika utendaji wa shirika lenye msimamo mkali.’ Akipatikana na hatia, anaweza kukabili kifungo cha miaka miwili hadi minne gerezani.

Februari 7, 2018, Belgorod: Kikundi kikubwa cha maofisa wa polisi kilivamia nyumba kumi hivi za Mashahidi. Maofisa waliwalazimisha baadhi ya wamiliki wa nyumba walale chini au waliwabana ukutani. Polisi walipekua nyumba zao na walipora vifaa vyao vya kielektroni, hati za kusafiria, picha, na pesa. Kisha, wakawapeleka Mashahidi kwenye kituo cha polisi, wakawahoji, na baada ya hapo wakawaachilia wote isipokuwa Anatoly Shalyapin na Sergei Voikov. Polisi waliwaweka kizuizini wanaume hao wawili kwa saa 48 na kisha wakawaachilia. Ingawa wameachiliwa, wanaume hao wamekatazwa kusafiri nje ya Belgorod.

Januari 23, 2018, Kemerovo: Polisi walivamia na kupekua nyumba 12 za Mashahidi na kupora vifaa vyao vyote vya kielektroni, machapisho yao ya kidini, na hati nyingi. Kabla ya kuvamiwa, mwanamume fulani aliyejifanya kuwa Shahidi wa Yehova alihudhuria mikutano ya Mashahidi na aliwarekodi kisiri, kisha akawapa polisi rekodi hizo. Kwa kutegemea rekodi hizo, wenye mamlaka walianza kufanya uchunguzi wa makosa ya uhalifu.

Uamuzi wa Mahakama Kuu Unaweza Kugawanya Familia

Katika hali hii isiyo na usawaziko ya matendo yanayofanywa na polisi pamoja na Maofisa wa Usalama wa Taifa, wenye mamlaka nchini Urusi wamekubaliana kwamba nchi iwachukue watoto wote wa Mashahidi wa Yehova kwa ajili ya “kuwarekebisha tabia.” Novemba 14, 2017, Baraza la Mahakama Kuu ya Shirikisho la Urusi lilitoa uamuzi, katika Maazimio Na. 44, kwamba wazazi wanaweza “kunyang’anywa na mahakama haki ya kulea watoto wao” ikiwa watawahusisha na shirika la kidini ambalo limepigwa marufuku kwa sababu ya “msimamo mkali.”

Novemba 23, 2017, Wizara ya Elimu na Sayansi ilitoa “mapendekezo” kwa nchi nzima ya kutaka watoto wanaoshirikiana na “falsafa ya dini zenye msimamo mkali” “warekebishwe tabia.” Wizara hiyo ilitaja watoto walio katika makundi mawili, yaani, watoto wa washiriki wa kundi la kigaidi la ISIS na watoto wa Mashahidi wa Yehova. Iligunduliwa kwamba “makumi ya maelfu ya watoto na matineja” ni wa Mashahidi wa Yehova. Kufikia sasa, hakuna mtoto aliyechukuliwa kutoka kwa wazazi wake.

Kampeni Hii ya Uvamizi Itaishia Wapi?

Hakuna nchi yoyote ambayo ni mwanachama wa Umoja wa Ulaya iliyofanya mashambulizi mabaya kama haya dhidi ya dini yenye amani ambayo ina wafuasi wachache. Mashahidi wa Yehova nchini Urusi hawawezi tena kuhudhuria ibada au kusoma na kujifunza Biblia hadharani. Ili wasikamatwe na kuteswa kama wahalifu, wanalazimika kufanya ibada kwa siri, kama walivyokuwa wakifanya wakati wa Muungano wa Sovieti.

Mashahidi wa Yehova ulimwenguni pote wanasikitishwa sana na hali inayowapata waabudu wenzao nchini Urusi na jinsi kampeni hiyo inayoongozwa na serikali itakavyowaathiri kihisia, kiroho, na kimwili. Philip Brumley, Wakili wa Mashahidi wa Yehova, alisema hivi: “Serikali ya Urusi inapaswa kuacha ukosefu huu wa haki na ifuate mikataba yake ya kimataifa ya kuheshimu haki za kibinadamu na uhuru wa kuabudu. Kwa kuwa wenye mamlaka wamemaliza kushambulia mashirika yao ya kisheria sasa wanawafunga gerezani Mashahidi wenyewe. Ni nini kitakachowapata Mashahidi wa Yehova nchini Urusi?”