DESEMBA 5, 2017
URUSI
Kesi Inayohusu Serikali Kupora Mali ya Ofisi ya Taifa ya Mashahidi Nchini Urusi Itaanza Kusikilizwa
Wenye mamlaka nchini Urusi wanatarajia kupora mali iliyotumiwa na Kituo cha Usimamizi cha Mashahidi wa Yehova, kilichopo Solnechnoye, karibu na St. Petersburg.
Uamuzi wa Mahakama Kuu wa Aprili 20, 2017, uliamuru kupigwa marufuku kwa mashirika yote ya kisheria ya Mashahidi na kutaifisha mali zake, kutia ndani mali zilizotumiwa na Kituo cha Usimamizi. Hata hivyo, mali zinazoleta utata ni zile zilizomilikiwa na shirika la kisheria la Marekani, yaani, Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania (WTPA). Lakini mwendesha mashtaka anajaribu kubatilisha mkataba uliofanywa miaka 17 iliyopita ambao ulibadili kisheria umiliki wa mali hizo ili ziwe mali ya WTPA. Mkataba huo haukuwa umepingwa kabla ya uamuzi wa Mahakama Kuu, na WTPA imekuwa ikilipa kodi tangu umiliki wa mali hiyo ulipobadilishwa. Wenye mamlaka wanajaribu mbinu za hila ili kuhalalisha malengo yao ya kupora mali hiyo.
Katika kesi ya awali iliyosikilizwa Novemba 29, 2017, hakimu alitoa nafasi kwa mwendesha mashtaka kwa kupuuza ombi la kufuta kesi hiyo lililotolewa na mawakili wa Mashahidi. Licha ya kupoteza mali yenye thamani ya pesa nyingi, Kituo kilikuwa makazi ya raia 400 wa Urusi na raia wa nchi nyingine, na baadhi yao wameishi hapo kwa miaka 20 au zaidi. Kuhamishwa kutoka katika makazi yao na kuvurugwa kwa utumishi wao wa kidini ambao walikuwa wakijitolea kuufanya kwa niaba ya raia wenzao wa Urusi kumekuwa pigo kubwa sana kwao.
Kesi hiyo itaanza kusikilizwa Desemba 7, 2017, saa 8:00 alasiri katika mahakama ya Wilaya ya Sestroretskiy jijini St. Petersburg.