Hamia kwenye habari

NOVEMBA 23, 2018
URUSI

Mashahidi Waendelea Kukamatwa na Kufungwa Nchini Urusi

Mashahidi Waendelea Kukamatwa na Kufungwa Nchini Urusi

Katika mwezi wa Oktoba 2018, polisi walivamia nyumba zaidi ya 30 kotekote magharibi ya Urusi. Ndugu sita na dada wawili walikamatwa na kuhukumiwa wabaki mahabusu kwa madai ya kushiriki utendaji wenye msimamo mkali. Kwa hiyo, sasa kuna ndugu na dada 25 waliofungwa gerezani isivyo haki, na 18 wengine wamehukumiwa kifungo cha nyumbani.

Oktoba 7, Sychyovka, Eneo la Smolensk—Polisi na askari wa kikosi maalum walioziba uso walipekua nyumba nne na kuwakamata dada wawili, Nataliya Sorokina mwenye umri wa miaka 43 na Mariya Troshina mwenye umri wa miaka 41. Siku mbili baada ya kuwakamata, Mahakama ya Wilaya ya Leninsky iliwahukumu dada zetu wabaki mahabusu hadi Novemba 19, 2018. Kisha, Novemba 16, 2018, Mahakama ya Wilaya ya Leninsky iliongeza muda wa dada hao kubaki mahabusu kwa miezi mitatu zaidi, yaani, mpaka Februari 19, 2019.

Oktoba 9, Kirov, Eneo la Kirov—Nyumba 19 hivi zilivamiwa. Wazee watano wa kutaniko walikamatwa na baadaye wakahukumiwa kubaki mahabusu. Wanne kati yao (Maksim Khalturin, Vladimir Korobeynikov, Andrey Suvorkov, na Evgeniy Suvorkov) ni raia wa nchi ya Urusi, na mmoja, Andrzej Oniszczuk, ni raia wa nchi ya Poland. Ndugu Oniszczuk ni mtu wa pili kutoka nchi nyingine kufungwa isivyo haki kwa sababu ya imani yake ya Kikristo, wa kwanza ni Dennis Christensen kutoka Denmark.

Oktoba 18, Dyurtyuli, Jamhuri ya Bashkortostan—Polisi walivamia nyumba 11 hivi na kupora pesa, kadi za benki, picha, barua, kompyuta, kadi za simu, na simu. Anton Lemeshev, ambaye ni mzee wa kutaniko, alikamatwa na kuhukumiwa abaki mahabusu kwa miezi miwili. Oktoba 31, 2018, aliachiliwa kutoka gerezani na kuhukumiwa kifungo cha nyumbani hadi sasa.

Licha ya vitisho vya kuvamiwa na kunyang’anywa mali zao isivyo haki, ndugu na dada wanaendelea kusali kwa ajili ya wale walio gerezani na kuwaandalia msaada inapowezekana wao pamoja na familia zao. Ndugu ulimwenguni pote wataendelea kusali kwa ajili ya watumishi waaminifu wa Yehova nchini Urusi, hata wakitaja baadhi yao kwa majina, mpaka hali zitakapobadilika.—Waefeso 6:18.