Hamia kwenye habari

MACHI 16, 2017
URUSI

Wizara ya Haki ya Urusi Inaelekea Kuwapiga Marufuku Mashahidi wa Yehova Nchini Urusi

Wizara ya Haki ya Urusi Inaelekea Kuwapiga Marufuku Mashahidi wa Yehova Nchini Urusi

Wizara ya Haki ya Urusi imefungua kesi kwenye Mahakama Kuu, ikitaka “shirika la kidini, yaani, Kituo cha Usimamizi cha Mashahidi wa Yehova, kitangazwe kuwa na msimamo mkali wa kidini, utendaji wake upigwe marufuku, na kituo hicho kifungwe.” Machi 15, 2017, Mahakama Kuu ilituma taarifa kwenye tovuti yake rasmi kwamba imepokea malalamiko kutoka kwenye Wizara ya Haki ya Urusi. Wizara hiyo haikuwapa taarifa Mashahidi wa Yehova kwamba imechukua hatua hiyo ya mwisho katika mashambulizi yanayoendelea dhidi ya ibada yao.

Ikiwa uamuzi wa Mahakama Kuu utaunga mkono madai ya wizara, hilo linaweza kuwa na matokeo mabaya sana kwa Mashahidi wa Yehova nchini Urusi. Mashahidi wanaweza kupoteza mali zote wanazozitumia kwa ajili ya ibada yao ya kidini, karibu mashirika 400 ya kidini yatafungwa, na huenda kila mmoja wa Mashahidi zaidi ya 170,000 atafikishwa mahakamani kwa sababu tu ya kuhudhuria mkutano wa kidini, kusoma Biblia pamoja, au kuzungumza na wengine kuhusu imani yao.

Vasiliy Kalin, mwakilishi wa Kituo cha Usimamizi nchini Urusi, alisema hivi: “Tamaa kuu ya kila Shahidi wa Yehova nchini Urusi ni kumwabudu Mungu wetu kwa amani. Sheria ya nchi ya Urusi inatupatia haki ya kufanya hivyo, lakini kwa zaidi ya miaka 100, wenye mamlaka nchini Urusi wamekiuka mambo yaliyohakikishwa katika sheria zao wenyewe. Nilikuwa mvulana mdogo wakati ambapo Stalin aliihamisha familia yetu kwenda Siberia kwa sababu tu sisi tulikuwa Mashahidi wa Yehova. Inahuzunisha na ni jambo la kulaumika kwamba watoto wangu na wajukuu zangu wanakabili hali kama hiyo. Sitarajii hata kidogo kwamba tungekuwa tukikabili tena tisho la kupatwa mateso kwa sababu ya ibada yetu katika Urusi ya kisasa.”