Hamia kwenye habari

JUNI 28, 2017
URUSI

Mahakama Imekataa Rufaa ya Kupinga Kuwekwa Mahabusu kwa Dennis Christensen

Mahakama Imekataa Rufaa ya Kupinga Kuwekwa Mahabusu kwa Dennis Christensen

Juni 21, 2017, Mahakama ya Mkoa ya Oryol ilikataa rufaa iliyokatwa kupinga kuwekwa mahabusu kwa Dennis Christensen. Bw. Christensen, raia wa Denmark, alikamatwa Mei 25, 2017 wakati wawakilishi wa Idara ya Usalama wa Taifa (FSB) walioziba nyuso zao na maofisa wa polisi waliokuwa na silaha walipovamia mkutano wa kidini wa Mashahidi wa Yehova.

Hivi karibuni, Mahakama Kuu ya Urusi ilitangaza kwamba mashirika yote ya kisheria ya Mashahidi wa Yehova nchini Urusi yana “msimamo mkali” na ilitoa hukumu ya kupiga marufuku utendaji wa mashirika hayo ya kisheria ya Mashahidi haraka iwezekanavyo. Maofisa waliovamia ibada ya Mashahidi Mei 25 waliwaambia wahudhuriaji kwamba wanaweza kufunguliwa mashtaka kwa kuendeleza utendaji wa shirika lililofungwa kwa sababu ya msimamo mkali. FSB waliiomba mahakama itoe amri kwamba Bw. Christensen awekwe mahabusu mpaka Julai 23, 2017—ingawa yeye ni raia mwenye amani, asiye na rekodi yoyote ya uhalifu—ili idara hiyo iwe na muda wa kutosha kutayarisha kesi dhidi yake, wakimshitaki kwa madai ya kuwa na msimamo mkali.

Mashahidi wa Yehova wamekata rufaa dhidi ya hukumu isiyo ya haki ya Mahakama Kuu na pia wanajitayarisha kutetea haki zao za kuendelea kuabudu kwa amani bila vizuizi vyovyote, kama inavyoelezwa kwenye Katiba ya Urusi na Mkataba wa Ulaya wa Haki za Kibinadamu.