Hamia kwenye habari

Hakimu Ivanenko wa Mahakama Kuu akitangaza uamuzi dhidi ya Mashahidi wa Yehova nchini Urusi

APRILI 21, 2017
URUSI

Mahakama Kuu Imeamua Utendaji wa Mashahidi wa Yehova Ni Kosa la Jinai Nchini Urusi

Mahakama Kuu Imeamua Utendaji wa Mashahidi wa Yehova Ni Kosa la Jinai Nchini Urusi

Aprili 20, 2017, licha ya shutuma kutoka ulimwenguni pote, Mahakama Kuu ya Urusi imetoa uamuzi wa kufanya utendaji wa Mashahidi wa Yehova uwe kosa la jinai nchini Urusi. Hakimu Yuriy Grigoryevich Ivanenko wa Mahakama Kuu alitoa hukumu iliyounga mkono madai yaliyotolewa na Wizara ya Haki ya “kuzuia utendaji wa kidini wa ‘Kituo cha Usimamizi cha Mashahidi wa Yehova nchini Urusi’ na mashirika yote ya kidini ambayo ni sehemu ya Kituo hicho. Mali zote zinazomilikiwa na Kituo cha Usimamizi zitakuwa za Shirikisho la Urusi.”

Hakimu Ivanenko aliendelea kueleza kwamba uamuzi huo unaoanza kutumika mara moja, unazuia utendaji wa mashirika yote ya kisheria ya Mashahidi nchini Urusi. Ingawa Mashahidi wa Yehova wamekata rufaa kwenye Mahakama Kuu ya Rufaa, uamuzi huo unapiga marufuku ibada yao.

Jopo la wanasheria wa Kituo cha Usimamizi

Vasiliy Kalin, ambaye alipokuwa na umri wa miaka minne alihamishwa kupelekwa Siberia pamoja na wazazi wake kwa sababu ya imani yao wakiwa Mashahidi wa Yehova, alisema hivi: “Tangu hukumu hiyo ilipotangazwa, maisha ya kila Shahidi wa Yehova nchini Urusi, iwe ni mtu mmoja au familia nzima, yamebadilika. Wote sasa wanakabili tisho la kuteswa kama wahalifu na kufungwa gerezani kwa sababu ya imani yao.”

Philip Brumley, Wakili Mkuu wa Mashahidi wa Yehova, alisema hivi: “Uamuzi uliofanywa leo umetuvunja moyo sana. Mtu anapochunguza maandishi yote na ushahidi uliotolewa anaona wazi kwamba kuna mkataa mmoja tu unaopatana na akili—kwamba Kituo cha Usimamizi hakikujihusisha kamwe na kile kinachodaiwa kuwa utendaji wenye msimamo mkali. Tunakata rufaa kupinga uamuzi huu.”