Hamia kwenye habari

OKTOBA 1, 2014
URUSI

Mashahidi Wakata Rufani Kwenye Mahakama Kuu ya Shirikisho la Urusi kwa Kufungwa kwa Shirika Lao la Kisheria Jijini Samara

Mashahidi Wakata Rufani Kwenye Mahakama Kuu ya Shirikisho la Urusi kwa Kufungwa kwa Shirika Lao la Kisheria Jijini Samara

Oktoba 8, 2014, Mahakama Kuu ya Shirikisho la Urusi itasikiliza kesi ya rufani ya Mashahidi wa Yehova jijini Samara kuhusu kufungwa kwa shirika lao la kisheria, Local Religious Organization (LRO). Awali, mahakama nyingine ndogo iliamua kwamba shirika la LRO jijini Samara lina msimamo mkali wa kidini. Ikiwa Mahakama Kuu haitafutilia mbali uamuzi huo, Mashahidi wa Yehova zaidi ya 1,500 wanaoishi jijini Samara watakabili hali ngumu sana.

Ofisi ya Mwendesha-Mashtaka ya Eneo la Samara Yatumia Mbinu za Uchokozi

Kesi dhidi ya LRO ilianza Aprili 2014, Ofisi ya Mwendesha-Mashtaka ya Eneo la Samara ilipofungua mashtaka kwenye Mahakama ya Eneo la Samara ili shirika hilo lifungwe kwa sababu ya shughuli za kidini zinazodaiwa kuwa na msimamo mkali. Hata kabla mahakama ya eneo haijasikiliza kesi hiyo, ofisi ya mwendesha-mashtaka ilifunga shirika hilo na kulipokonya mali zake kwa muda. Uamuzi huo ulipofanywa, na hata kabla ya kesi kuanza, Wizara ya Sheria ya Shirikisho la Urusi iliweka LRO kwenye orodha ya mashirika ya kidini ambayo utendaji wake umepigwa marufuku kwa sababu ya msimamo mkali. Kisha, Mei 29, 2014, Hakimu Shabayeva akafanya uamuzi unaopendelea ofisi ya mwendesha-mashtaka na kuamuru shirika hilo lifungwe na mali zake zichukuliwe.

Hiyo si mara ya kwanza kwa Ofisi ya Mwendesha-Mashtaka ya Eneo la Samara kupeleka kesi mahakamani ili shirika la LRO lifungwe. Mwaka wa 2009, ofisi hiyo ya mwendesha-mashtaka ilifungua mashtaka lakini baadaye ikayaondoa mahakamani. Katika kisa cha sasa, mamlaka za kutekeleza sheria jijini Samara zilibadilisha mbinu ili zitimize lengo lake.

Mahakama za Urusi Zafunga LRO kwa Sababu Zisizo na Msingi

Mnamo Januari 2013 na Januari 2014, polisi walifanya msako kwenye majengo ambayo Mashahidi hukodisha kwa ajili ya ibada na kudai walipata machapisho yaliyo kwenye Orodha ya Serikali ya Vitabu Vinavyowachochea Watu Kuwa na Msimamo Mkali wa Kidini. Ofisi ya Mwendesha-Mashtaka Jijini Samara ilitoa onyo kwa LRO kuhusu msako huo wa mwaka wa 2013, na polisi walipopata tena machapisho ya kidini Januari mwaka wa 2014, ofisi hiyo ililishtaki shirika hilo. Machi 7, 2014, Mahakama ya Wilaya ya Sovetskiy jijini Samara ilisema shirika la LRO lina hatia na ikalitoza faini ya dola 1,383 za Marekani (rubo 50,000). Mashahidi jijini Samara wanajua kwamba katika misako yote miwili, polisi ndio walioleta machapisho waliyosingizia kuwa yalipatikana. Isitoshe, Mashahidi wa Yehova hawajakubaliana na uamuzi wa Mahakama za Urusi uliotangaza kwamba machapisho hayo yanawachochea watu kuwa na msimamo mkali wa kidini, na basi wamekata rufani kwenye Mahakama ya Ulaya ya Haki za Kibinadamu.

Baada ya Mahakama ya Ofisi ya Mwendesha-Mashtaka ya Eneo la Samara kuungwa mkono na Mahakama ya Wilaya ya Sovetskiy, ilifungua pia kesi kwenye Mahakama ya Eneo la Samara kuhusu mashtaka ya kuwa na msimamo mkali wa kidini. Hizo zilikuwa mbinu za kufunga shirika la kisheria la Mashahidi katika eneo hilo. Mawakili wa Mashahidi walimweleza Hakimu Shabayeva kwamba hakukuwa na sababu ya msingi ya kufunga LRO na kwamba utendaji, imani ya Mashahidi wa Yehova, na pia shirika la LRO halina msimamo mkali wa kidini. Walimweleza pia kwamba polisi ndio walioleta “machapisho yaliyopigwa marufuku” yanayodaiwa kuwa yalipatikana wakati wa msako. Hata hivyo, Hakimu Shabayeva aliamua kufunga shirika la kisheria la Mashahidi jijini Samara.

Je, Mamlaka za Urusi Zitaendelea Kuwanyima Watu Uhuru wa Kuabudu?

Kisa hicho cha Samara kinafanana na hatua zilizochukuliwa na wenye mamlaka dhidi ya Mashahidi wa Yehova jijini Taganrog, ambako kwa mara ya kwanza, mamlaka zilitumia kwa njia isiyofaa Sheria ya Kudhibiti Vikundi Vyenye Msimamo Mkali ya Serikali ya Urusi kuhusiana na ibada ya Mashahidi. Mamlaka zilifaulu kufunga LRO ya jiji la Taganrog mwaka wa 2009, na baadaye zikashtaki Shahidi mmoja-mmoja kama mhalifu. Mashtaka ya uhalifu hatimaye yalifanya Mashahidi saba wa eneo hilo wapatikane na hatia kwa sababu tu ya kuhudhuria mikutano ya ibada. Mashahidi jijini Samara wanahofia kwamba huenda uamuzi huo ukawa na matokeo sawa na hayo.

Mamlaka nchini Urusi zitaendelea kushambulia ibada ya Mashahidi wa Yehova jinsi hiyo hadi lini? Tangu Juni 2014, Mashahidi wamefunguliwa mashtaka bandia katika maeneo mbalimbali nchini Urusi kwa sababu ya kugawanya machapisho yanayodaiwa kuwachochea watu kuwa na msimamo mkali wa kidini. Mashahidi wa Yehova jijini Samara wanatumaini kwamba Mahakama Kuu ya Shirikisho la Urusi itatekeleza haki katika kesi yao.