APRILI 19, 201
URUSI
Siku ya Tano ya Kesi Katika Mahakama Kuu ya Urusi: Mashtaka ya Miaka Kumi Dhidi ya Mashahidi Yakaguliwa
NEW YORK—Jumatano, Aprili 19, 2017, watu 300 hivi walikusanyika kwenye Mahakama Kuu ya Shirikisho la Urusi (wengine walifika mapema sana kama saa 8:00 usiku) kwa ajili ya siku ya tano ya kusikilizwa kwa madai ya Wizara ya Haki kwamba Kituo cha Usimamizi cha Mashahidi wa Yehova kifungwe. Muhtasari ulitolewa wa matendo ya ukatili yaliyofanywa na wenye mamlaka wa Urusi dhidi ya Mashahidi wa Yehova katika miaka kumi iliyopita baada ya Mahakama kukagua mabuku 43 yaliyojaa hati zilizowasilishwa kama stakabadhi za kesi hiyo.
Muhtasari huo ulipokuwa ukiendelea kutolewa, mawakili wanaoiwakilisha Wizara ya Haki hawangeweza kuonyesha msingi hususa wa kisheria wa kutaka Kituo cha Usimamizi kifungwe wala hawakuweza kuonyesha utendaji wowote wenye msimamo mkali unaoendelezwa na Kituo cha Usimamizi au na yoyote kati ya mashirika ya Local Religious Organizations (Mashirika ya Kidini ya Mashahidi wa Yehova au LRO) yanayotumiwa na Mashahidi wa Yehova nchini Urusi. Yuri Toporov, mmoja wa mawakili wa Kituo cha Usimamizi, aliiambia Mahakama kwamba miongoni mwa stakabadhi zilizowasilishwa katika kesi hiyo, kuna tuzo na barua za uthamini ambazo Kituo cha Usimamizi kilipokea kutoka serikalini, jambo linaloonyesha kwamba kwa miaka kadhaa Kituo cha Usimamizi kilitambuliwa na wenye mamlaka kwa kuisaidia jamii. Pia, ilionekana wazi kwamba LRO zinaisaidia jamii katika njia hiyo. Isitoshe, mabuku kadhaa ya stakabadhi za kesi zinaonyesha kwamba Wizara ya Haki imekuwa ikichunguza LRO zinazotumiwa na Mashahidi nchini Urusi tangu 2008 lakini haijawahi kupata utendaji wowote wenye msimamo mkali katika LRO hizo, jambo ambalo lilikubaliwa na mawakili wa Wizara ya Haki.
Mahakama itaendelea kusikiliza kesi hiyo Aprili 20, 2017, saa 8:00 alasiri.
Wanahabari Wanaweza Kuwasiliana na:
David A. Semonian, Ofisi ya Habari za Umma, +1-845-524-3000
Urusi: Yaroslav Sivulskiy, +7-911-087-8009