Hamia kwenye habari

JANUARI 23, 2015
URUSI

Uamuzi wa Mahakama Kuu ya Shirikisho la Urusi Wahatarisha Uhuru wa Kidini wa Mashahidi Nchini Urusi

Uamuzi wa Mahakama Kuu ya Shirikisho la Urusi Wahatarisha Uhuru wa Kidini wa Mashahidi Nchini Urusi

Novemba 12, 2014, Mahakama Kuu ya Shirikisho la Urusi ilitetea uamuzi wa mahakama ndogo iliyoamua kwamba Shirika la Kisheria la Mashahidi wa Yehova la Samara, Local Religious Organization (LRO) lina msimamo mkali wa kidini. Ofisi ya mwendesha-mashtaka ya Samara ilifungua kesi dhidi ya Shirika la LRO mwaka wa 2014 baada ya polisi kufanya msako kwenye majengo ambayo Mashahidi walikodisha kwa ajili ya mikutano na “kupata” machapisho kadhaa ya kidini yaliyokuwa yamepigwa marufuku kotekote nchini. Awali machapisho hayo yalikuwa yamepigwa marufuku na mahakama za Urusi kwa sababu eti ni yenye msimamo mkali wa kidini na kuwekwa kwenye Orodha ya Serikali ya Vitabu na Habari Zinazowachochea Watu Kuwa na Msimamo Mkali wa Kidini. a Hata hivyo, Mashahidi wa Samara tayari walikuwa wameyaondoa machapisho hayo kutoka katika majengo waliyokodi kwa ajili ya ibada, kwa kutii maamuzi hayo ya mahakama.

Mashahidi walieleza mahakama ndogo na Mahakama Kuu kwamba polisi waliofanya msako ndio walioweka machapisho hayo yaliyopigwa marufuku katika majengo yao ya ibada ili kutafuta msingi wa kuwafungulia mashtaka. Mashahidi walieleza pia kwamba Mahakama ya Ulaya ya Haki za Kibinadamu kwa sasa bado inachunguza uhalali wa maamuzi ya awali ya mahakama ya Urusi ya kupiga marufuku baadhi ya machapisho yao. Zaidi ya hilo, Mashahidi walieleza kwamba hata ikiwa madai ya mwendesha-mashtaka yalikuwa ya kweli, kwamba Mashahidi walihifadhi machapisho yaliyopigwa marufuku, bado adhabu iliyotolewa hailingani na kosa hilo dogo. Kosa la kuhifadhi machapisho yaliyopigwa marufuku lina adhabu ya kulipa faini au kufunga kwa muda utendaji wa LRO, na si kufunga kabisa utendaji wa shirika hilo. Hata hivyo, Mahakama Kuu haikuzingatia maelezo hayo.

Je, Kufungwa kwa Shirika la Kisheria (LRO) Kutaongoza Kwenye Shtaka la Kosa la Uhalifu?

Kesi hiyo ya kufungwa kwa shirika la LRO la Samara inafanana na kesi katika jiji la Taganrog, ambapo Mahakama ya Mkoa wa Rostov iliamuru kufungwa kwa shirika la LRO la jiji hilo mwaka wa 2009 kwa madai ya kuwa na msimamo mkali wa kidini. Hivyo, mamlaka za kutekeleza sheria jijini Taganrog zilitumia uamuzi huo kama kigezo cha kupiga marufuku utendaji wa kidini wa Mashahidi wa Yehova katika eneo hilo. Mwaka wa 2013, Mashahidi kumi na sita wa Taganrog walishtakiwa kosa la uhalifu kwa sababu ya utendaji wao wa kidini, utendaji uleule unaofanywa na Mashahidi ulimwenguni pote, kutia ndani Samara. Mashahidi saba walitozwa faini kubwa; wanne kati yao ambao ni wazee makutanikoni, walihukumiwa pia vifungo virefu gerezani. Hata hivyo, hakimu aliondoa faini hizo kwa sababu kulingana na sheria, muda mrefu mno ulikuwa umepita tangu waliposhtakiwa na akaahirisha vifungo vyote vya gerezani. Mashahidi wamekata rufani kuhusiana na mashtaka hayo, na Desemba 12, 2014, Mahakama ya Mkoa ya Rostov iliagiza kesi isikilizwe upya na hakimu mwingine.

Mashahidi wa Yehova 1,500 wanaoishi eneo la Samara wako katika hatari ya kushtakiwa makosa ya uhalifu kwa sababu ya kuabudu. Mwisho wa kesi hizi utakuwa upi? Serikali ya Urusi pia inachunguza mashirika ya LRO ya Mashahidi katika sehemu mbalimbali nchini humo. Tunasubiri kuona jinsi ambavyo matukio hayo yenye kukandamiza yatakavyowaathiri Mashahidi 180,000 wanaoishi Urusi. Hata hivyo, uamuzi huo wa Mahakama Kuu unahatarisha uhuru wa kidini wa Mashahidi wa Yehova na dini nyingine ndogondogo nchini Urusi.

a Kufikia sasa, machapisho 73 ya kidini ya Mashahidi wa Yehova yamewekwa katika Orodha ya Serikali ya Vitabu na Habari Zinazowachochea Watu Kuwa na Msimamo Mkali wa Kidini. Miongoni mwa machapisho yaliyopatikana katika jengo lililokodishwa na shirika la LRO la Samara ni kitabu Mwabudu Mungu wa Pekee wa Kweli. Kimechapishwa katika lugha 158 na nakala 23,970,207 za kitabu hicho zimegawanywa. Kitabu kingine kilichopatikana ni Ujuzi Uongozao Kwenye Uhai Udumuo Milele, ambacho kimechapishwa katika lugha 166 na nakala 100,944,355 zimesambazwa. Mashahidi wa Yehova wamefungua kesi katika Mahakama ya Ulaya ya Haki za Kibinadamu kupinga maamuzi ya mahakama za Urusi zinazodai kuwa machapisho yao ni yenye msimamo mkali wa kidini.