MACHI 3, 2014
URUSI
Mahakama ya Rufani ya Urusi Yatetea Haki za Kibinadamu kwa Kukataa Kupiga Marufuku JW.ORG
Januari 22, 2014, mahakimu watatu wa Mahakama ya Mkoa wa Tver walibatilisha uamuzi uliokuwa umetolewa na Mahakama ya Wilaya, uamuzi wa kupiga marufuku jw.org—tovuti rasmi ya Mashahidi wa Yehova. a Mahakama hiyo ya Mkoa ilitenda tofauti kabisa na maamuzi mengine yaliyokuwa yametolewa miaka michache iliyopita na mahakama za Urusi. Ilitenda kinyume na matarajio kwa kufuata sheria ipasavyo ilipokataa kutekeleza jitihada nyingi za mwendesha mashtaka za kupiga marufuku tovuti hiyo.
Unyanyasaji na ukatili huo ulioungwa mkono na serikali ya Urusi ulichukua mkondo hatari Agosti 7, 2013, mahakama ya wilaya (iliyoko kilomita 160 kaskazini magharibi mwa Moscow) ilipoamua kupiga marufuku jw.org katika kesi iliyochukua dakika 25 tu. Wawakilishi wa Mashahidi wa Yehova hawakujulishwa kuhusu siku ya kesi hiyo na hawakupewa nafasi ya kujitetea dhidi ya madai yaliyokuwa yametolewa na mwendesha mashtaka wa mahakama hiyo ya wilaya. Mashahidi wa Yehova walisikia kupitia vyombo vya habari, uamuzi uliokuwa umetolewa wa kupiga marufuku tovuti yao nchini Urusi, saa chache tu kabla ya muda waliotarajiwa kukata rufani uishe, Septemba 12, 2013. Mara moja walikata rufani kwenye Mahakama ya Mkoa wa Tver.
Mahakama ya Mkoa iliposikiliza rufani hiyo, Januari 22, 2014, ilitambua kwamba haki za wamiliki wa tovuti hiyo, Watchtower Bible and Tract Society of New York, Inc., zilikuwa zimekiukwa na ikaagiza kesi hiyo isikizwe upya na pande zote zipewe nafasi ya kujieleza. Akiungwa mkono na wawakilishi kutoka Wizara ya Haki na Wizara ya Mambo ya Ndani, mwendesha mashtaka wa mahakama ya wilaya aliiomba mahakama itangaze kwamba tovuti ya jw.org ni tovuti yenye “msimamo mkali wa kidini” na hivyo ipigwe marufuku kotekote nchini Urusi. Mahakama hiyo ya Mkoa ilipinga madai yake.
Kampeni ya unyanyasaji yaanza nchini kote—sheria ya msimamo mkali wa kidini yatumiwa vibaya ili kuzuia kazi ya Mashahidi wa Yehova. Kuanzia mwaka wa 2009, wenye mamlaka nchini Urusi walitumia kifungu cha maneno yasiyoeleweka vizuri kinachopatikana katika Sheria ya Serikali ya Kupambana na Watu Wenye Msimamo Mkali, ili kuzidisha unyanyasaji si tu kwa Mashahidi wa Yehova wachache waliotawanyika sehemu mbalimbali nchini Urusi, bali kwa Mashahidi wote nchini humo. Wenye mamlaka wameitumia vibaya sheria hiyo ili kutetea:
kukamatwa kwa Mashahidi wa Yehova zaidi ya 1,600;
kupiga marufuku machapisho 70 ya Mashahidi wa Yehova;
kufanya upekuzi katika nyumba 171 za watu binafsi na za ibada; na
kuvuruga au kukatiza mikutano ya ibada 69 kufikia sasa.
Kwenye kesi ya Mahakama ya Wilaya ya Tver, mwendesha mashtaka alitaka tovuti ya jw.org ipigwe marufuku kwa sababu ina machapisho sita yanayodaiwa kuwa yenye “msimamo mkali wa kidini.” Mahakama hiyo ilitumia sheria hiyo kufikia uamuzi wa Agosti 7, 2013 wa kupiga marufuku tovuti ya jw.org na kuijumlisha kwenye Orodha ya Serikali ya Vitabu na Habari Zinazowachochea Watu Kuwa na Msimamo Mkali wa Kidini.
Uamuzi wa mahakama haukupatana hata kidogo na kusudi lake kwa kuwa haukupendekeza njia nyingine ya kushughulikia suala hilo—kama vile kuagiza kuondolewa kwa machapisho yanayodaiwa kuwa na “msimamo mkali wa kidini” kutoka kwenye tovuti hiyo. Mahakama ya Mkoa ilipojua kwamba wamiliki wa tovuti hiyo walikuwa tayari wameondoa machapisho yote yanayodaiwa kuwa na “msimamo mkali wa kidini” kutoka kwenye tovuti hiyo nchini Urusi, iliamua moja kwa moja kwamba hakukuwa na sababu zozote za kisheria za kupiga marufuku tovuti hiyo. Huo ulikuwa uamuzi wa mwisho, ingawa mwendesha mashtaka ana kipindi cha miezi sita cha kukata rufani ya kutaka uamuzi huo ufutiliwe mbali.
Je, uamuzi uliotolewa na Mahakama ya Mkoa wa Tver unaashiria kwamba kuna mambo mema yanayokuja?
Tatizo bado lingalipo. Uchanganuzi na uamuzi wa Mahakama ya Mkoa ya Tver ni tofauti kabisa na uamuzi uliotolewa na mahakama nyinginezo nchini Urusi uliokusudiwa kuwakandamiza Mashahidi wa Yehova. Mahakama ya Ulaya ya Haki za Kibinadamu (ECHR) imekuwa ikiishutumu mara kadhaa nchi ya Urusi kwa kuukandamiza uhuru wa kidini wa Mashahidi wa Yehova. Badala ya kuunga mkono maamuzi ya ECHR, nchi ya Urusi imeendelea kukiuka haki za kibinadamu kwa kiwango kikubwa zaidi. Kwa sasa, Mashahidi wa Yehova wamewasilisha kesi 23 dhidi ya nchi ya Urusi kwenye Mahakama ya ECHR katika jitihada za kutetea uhuru wao wa ibada.
Je, uamuzi uliotolewa na Mahakama ya Mkoa wa Tver unaashiria kwamba kuna mambo mema yanayokuja? Mashahidi wa Yehova watafuatilia kwa ukaribu jambo hilo waone jinsi Urusi itakavyoitikia uamuzi huu na maamuzi mengine yatakayotolewa katika siku zijazo na Mahakama ya Ulaya ya Haki za Kibinadamu (ECHR).
a Ikiwa mahakama ingepiga marufuku tovuti ya jw.org kampuni zinazotoa huduma za Intaneti nchini Urusi zingelazimika kuwazuia watu wasiitembelee. Wenye mamlaka wangekuwa na uwezo wa kumfungulia mashtaka ya uhalifu mtu yeyote anayeitumia na hata anayewatia wengine moyo wafanye hivyo.