Hamia kwenye habari

JULAI 2, 2013
URUSI

Mahakama ya Ulaya Yalinda Haki ya Faragha Katika Kesi Inayohusu Mashahidi wa Yehova

Mahakama ya Ulaya Yalinda Haki ya Faragha Katika Kesi Inayohusu Mashahidi wa Yehova

NEW YORK—Mnamo Alhamisi, Juni 6, 2013, Mahakama ya Ulaya ya Haki za Kibinadamu (ECHR) iliagiza nchi ya Urusi ilipie hasara ya euro 5,000 (au dola za Marekani 6,622) kwa Bi. V. Zhukova na Bi. Y. Avilkina. Wenye mamlaka nchini Urusi walichukua rekodi za kibinafsi za kitiba za Bi. Zhukova na Bi. Avilkina bila idhini yao. Mahakama ilifikia uamuzi kwamba tendo hilo lilikiuka haki za kimsingi za kuwa na faragha, ambayo ni “kanuni muhimu sana” inayotegemezwa na Mkataba wa Ulaya.

Uamuzi huo wa mahakama ulifanywa baada ya kipindi cha miaka mitano cha kushughulikia kesi hiyo. Katika mwaka wa 2007, Naibu wa Kiongozi wa Mashtaka wa Jiji la St. Petersburg aliamuru kwamba mashirika ya kitiba katika mji huo yawasilishe “ombi lolote ambalo Mashahidi wa Yehova watatoa la kutotiwa damu mishipani au sehemu yoyote ya damu” na wayalete maombi hayo kwa ofisi ya kiongozi wa mashtaka bila kuwaambia mapema au kupata kibali cha mgonjwa. Hivyo, Machi 9, 2009, Mashahidi waliwasilisha kesi inayohusu Avilkina na Wengine dhidi ya Urusi kwa Mahakama ya Ulaya ya Haki za Kibinadamu. Katika uamuzi wake, Mahakama hiyo ilisema kwamba hatua iliyochukuliwa na nchi ya Urusi ilikuwa ya “ukandamizaji” na kwamba hakukuwa na “sababu halali na za kutosha” za kuwapa wenye mamlaka habari hizo za siri za kitiba.

Alipokuwa akizungumza kuhusu matokeo mazuri ambayo yamepatikana kutokana na kesi hiyo, Grigory Martynov, msemaji wa Mashahidi wa Yehova nchini Urusi alisema: “Uamuzi huo wa Mahakama unawahakikishia raia wa Urusi, kutia ndani wengine katika Baraza la Ulaya, kwamba haki zao za msingi zitalindwa.”

Wanahabari Wanaweza Kuwasiliana na:

J. R. Brown, Ofisi ya Habari za Umma, simu +1 718 560 5000

Urusi: Grigory Martynov, simu +7 812 702 2691