DESEMBA 11, 2017
URUSI
Mahakama ya Urusi Yafungua Njia ya Kupora Ofisi ya Taifa ya Mashahidi
Desemba 7, 2017, Mahakama ya Wilaya ya Sestroretskiy ilitoa uamuzi uliomuunga mkono mwendesha-mashtaka na ilibatilisha mkataba wa muda mrefu wa mali iliyokuwa ikitumiwa na Kituo cha Usimamizi cha Mashahidi wa Yehova nchini Urusi. Ikiwa uamuzi huu utaungwa mkono wakati wa rufaa, utafanya wenye mamlaka nchini Urusi waweze kuhalalisha kisheria uporaji wa mali hiyo iliyoko Solnechnoye, karibu na St. Petersburg.
Miaka kumi na saba iliyopita, umiliki wa mali hiyo ulibadilishwa kwa mkataba halali wa kisheria, nayo ikamilikiwa na Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania (WTPA), shirika la kisheria la Marekani, mkataba ambao haujawahi kupingwa na maofisa wa Urusi. WTPA ilitoa mali hiyo itumiwe na Kituo cha Usimamizi kwa ajili ya shughuli za kidini za Mashahidi wa Yehova nchini Urusi na ilikuwa ikilipa kodi kwa ajili ya mali hiyo.
Kufuatia uamuzi wa Aprili 20, 2017, wa Mahakama Kuu wa kufunga mashirika yote ya kisheria, kupiga marufuku utendaji wake, na kutaifisha mali zote za mashirika hayo; mwendesha-mashtaka sasa anadai kwamba mkataba huo wa miaka 17 haukuwa halali. Muda wa kupinga mkataba huo ulipita miaka mingi iliyopita. Baada ya kusikiliza kesi hiyo kwa saa nne wakati Mashahidi walipowasilisha ushahidi wa kutosha unaothibitisha kwamba badiliko hilo la umiliki wa mali lilikuwa halali kisheria na kwamba linapaswa kutambuliwa, Hakimu Bogdanova alitangaza uamuzi wa mahakama ambao uliunga mkono madai ya mwendesha-mashtaka.
Mashahidi wamepewa siku 30 za kuwasilisha rufaa.