MACHI 3, 2014
URUSI
Habari Zaidi: Jaribio la Kupiga Marufuku JW.ORG Lagonga Mwamba
ST. PETERSBURG, Urusi—Januari 22, 2014, Mashahidi wa Yehova walipata ushindi mkubwa katika kesi dhidi yao wakati mahakama ya rufani ilipobatilisha uamuzi uliofanywa na mahakama ya wilaya ya kupiga marufuku tovuti rasmi ya Mashahidi wa Yehova, kotekote nchini Urusi.
Mahakama ya Mkoa wa Tver ilibatilisha uamuzi uliofanywa Agosti 7, 2013 na Mahakama ya Wilaya ya Tsentralniy. Mahakama hiyo ya mkoa ilifikia uamuzi kwamba mahakama ya wilaya haikutenda kwa haki ilipoamua kwamba tovuti rasmi ya Mashahidi wa Yehova ipigwe marufuku, kwani Mashahidi ambao ndio wachapishaji wa tovuti hiyo hawakuhusishwa katika mazungumzo hayo. Kiongozi wa mashtaka wa Tver aliiwasilisha kesi hiyo mahakamani kwa sababu tovuti ya jw.org ina machapisho ambayo yalikuwa yameamuliwa na mahakama za Urusi kuwa yana “msimamo mkali sana wa kidini.” Baada ya kufahamu kuhusu uamuzi wa mahakama ya wilaya, Mashahidi wa Yehova waliondoa machapisho hayo kutoka kwenye tovuti ya jw.org ya lugha ya Kirusi. Mahakama ya Mkoa wa Tver ilikata kauli kwamba Mashahidi walifuata sheria za nchi ya Urusi na basi marufuku hiyo ikaondolewa.
Mashahidi wa Yehova wamechukua hatua za kisheria ili kutetea baadhi ya machapisho yaliyomo ndani ya tovuti yao, machapisho ambayo kulingana na mahakama za Urusi, yametangazwa kuwa yana “msimamo mkali sana wa kidini.” Wamepeleka maombi kadhaa ya kesi yao kwenye Mahakama ya Ulaya ya Haki za Kibinadamu ili kubatilisha uamuzi wa mahakama za Urusi.
Grigory Martynov, msemaji wa Mashahidi wa Yehova nchini Urusi, anasema: “Tunafurahi sana kwamba mahakimu waliona manufaa ya tovuti yetu na jitihada zetu za kuunga mkono maamuzi yaliyotolewa na mahakama za Urusi. Tutaendelea kutetea ubora wa machapisho yetu na pia haki ya raia wa Urusi ya kufaidika kikamili kutokana na kazi yetu ya kuwaelimisha watu kuhusu Biblia.”
“Mashahidi kote duniani wamefurahishwa sana na uamuzi huo,” anasema J. R. Brown, msemaji wa Mashahidi wa Yehova katika makao yao makuu ya ulimwenguni pote. “Kwa sababu ya uamuzi huo wa kisheria raia wote wa Urusi wataendelea kunufaika na tovuti hii bora ya kuwafundisha watu Biblia.”
Wanahabari Wanaweza Kuwasiliana na:
J. R. Brown, Ofisi ya Habari za Umma, simu +1 718 560 5000
Urusi: Grigory Martynov, simu +7 812 702 2691